Apr 28, 2024 04:26 UTC
  • UN yaunga mkono maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu Marekani ya kuwatetea watu wa Gaza

Stephen Dujaric Msemaji wa Umoja wa Mataifa jana Ijumaa alisema katika radiamali yake kwa maandamano yanayoendelea kufanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu huko Marekani katika kuwaunga mkono watu wa Gaza na kupinga mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo hilo kwamba: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni mfuasi na mungaji mkono mkubwa wa uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na huko Marekani; na anaunga mkono haki ya wananchi ya kufanya maandamano kwa amani.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametangaza kuwa inapasa kuhakikisha kuwa maandamano haya hayageuki na kuwa utowaji wa kauli za chuki. 'Tupo katika kipindi nyeti." Wakuu wa vyuo vikuu wanakabiliwa na wakati mgumu, na wanapasa kuweka sawa masuala yote haya', amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Stephane Dujarric, Msemaji wa UN

Hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuunga mkono maandamano ya amani nchini Marekani licha ya kutofurahishwa serikali ya Biden na pia Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kufuatia kuongezeka pakubwa maandamano na malalamiko ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo kwa lengo la kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa eneo hilo inaonyesha kuwa, taasisi hiyo ya kimataifa pia inaamini ulazima wa kuwepo uhuru wa kujieleza na kufanyika maandamano ya amani na kuwekwa kando vigezo vya undumakuwili kuhusu suala hili vinavyotekelezwa na Washington. Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amewataja waungaji mkono wa Wapalestina katika vyuo viku nchini Marekani kuwa wana chuki dhidi ya Uyahudi. Ameyataja maandamano hayo kuwa ya kutisha na kusema yanapasa kusitishwa." 

Wanafunzi wa matabaka mbalimbali katika vyuo vikuu vya Marekani wameonyesha mshikamano na kuwaunga mkono pakubwa watu wa Gaza, na wakati huo huo kupinga vikali sera za serikali ya Biden ya kuuhami kwa pande zote utawala haramu wa Israel. Vuguvugu la nchi nzima kwa jina la "Solidarity Movement with Gaza" lilianza kufanya maandamano ya kuiunga mkono Palestina kutokea Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga vita vya Israel huko Gaza, ambavyo vimesababisha kuuliwa shahidi makumi ya maelfu ya watu na kujeruhiwa wengine wengi miongoni mwao katika eneo hilo; na sasa maandamano hayo yameenea katika vyuo vikuu vingine huko Marekani, ambapo wanafunzi na wafanyakazi wa kada ya elimu zaidi ya 550 wametiwa mbaroni. 

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia wakipambana na polisi ya Marekani 

Marekani nchi ambayo inajigamba kuwa moja ya watetezi wakuu wa uhuru na haki za binadamu ulimwenguni, ukiwemo uhuru wa kujieleza inazuia kufanyika maandamano na mikusanyiko dhidi ya Israel ndani ya Marekani. Kitendo hiki kinaonyesha kuwa suala la uhuru wa kusema linaruhusiwa tu na serikali ya Marekani pale linapokuwa linaunga mkono na kutetea  sera za Washington na waitifaki wake hususan utawala wa Kizayuni. Kinyume chake, watu binafsi au taasisi hazipewi nafasi ya kuwasilisha mitazamo na maoni yao au kupinga sera tawala za nchi.  

Kwa kuzingatia kufanyika maandamano ya kuwaunga mkono raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza na kushuhudiwa malalamiko dhidi ya Israel katika vyuo vikuu zaidi ya 11 vya Marekani katika majimbo tofauti ya nchi hiyo yakiwemo ya New York, California, Texas na Massachusetts, serikali ya Washington imeomba msaada kwa polisi na vikosi vingine vya usalama kama kikosi cha gadi ya taifa kwa ajili ya kukabiliana na maandaano hayo ambayo yanafanyika kwa amani kabisa. Si hayo, tu, bali serikali ya Marekani imewatia nguvuni mamia ya wanafunzi na pia wafanyakazi wa kada mbalimbali za kielimu wa vyuo vikuu. Televisheni ya al Jazeera katika ripoti ya kuvutia imezungumzia taathira za uhuru wa kujieleza nchini Marekani yaani kuwaweka katika orodha nyeusi wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia waliofukuzwa na pia kuwauzia kuendelea na masomo na ajira na kueleza kuwa: Chuo Kikuu cha Columbia kina uhusiano wa karibu wa kiuchumi na Wall Street na kampuni za silaha zinazoiunga mkono Israel na kwamba wanafunzi na wahadhiri waliofukuzwa wanapoteza fursa ya kuendelea na masomo katika vyuo vikuu vingine na kuingia kwenye soko la ajira. Wiki iliyopita, zaidi ya wanafunzi 100 wanaounga mkono Palestina waliokuwa wamekusanyika katika Chuo Kikuu cha Columbia walitiwa mbaroni. Wanafunzi kadhaa pia wamesimamishwa masomo na kuwasilishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya chuo. 

Polisi wa Marekani wakikandamiza maandamano ya vyuo vikuu ya kuiunga mkono Palestina 

Bila shaka, vigezo vya undumakuwili vya Marekani ni vya kweli si tu katika suala la uhuru wa kujieleza bali pia katika uwanja wa haki za binadamu. Hii ni katika hali ambayo Washington inaendelea kukanusha juu ya kujiri mauaji yoyote ya kimbari huko Gaza licha ya kuwa kuna ushahidi usiopingika kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel.  

Shirika la Haki za Binadamu la Ulaya la Euro Mediterania limeashiria kugunduliwa makaburi ya umati zaidi ya 140 huko Ukanda wa Gaza na kutangaza kuwa miili mingi ya Wapalestina imezikwa ikiwa vipande vipande kwenye makaburi hayo, na kwamba inapaswa kuundwa kamati ya uchunguzi ya kimataifa ili kufuatilia jinai hiyo ya kutisha ya Israeli. 

Katika upande mwingine, utawala wa Kizayuni unazusha baa la njaa bandia katika Ukanda wa Gaza kwa kuwaua kwa njaa kwa makusudi watu wa eneo hilo. Pamoja na hayo lakini serikali ya Biden inapuuza jinai hizo na kukataa kuchukua hatua zozote madhubuti za kuzuia kuendelea ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel. 

Kwa hiyo,  Marekani inapasa kuhesabiwa kuwa mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika jinai zake ambazo hazijawahi kushuhudiwa tena dhidi ya Wapalestina wa Ukanda Gaza, kutokana na uungaji mkono kamili wa kisiasa, kidiplomasia na kijeshi na kiusalama wa nchi hiyo kwa  Tel Aviv, pamoja na kukandamiza maandamano yanayopinga Uzayuni yanayoendelea kushuhudiwa ndani ya Marekani.  

Tags