May 09, 2024 07:26 UTC
  • Kaburi jingine la umati lafukuliwa huko Gaza,

Wahudumu wa afya kaskazini mwa Gaza wametoaa miili mingine katika kaburi jingine la umati katika Hospitali ya Shifa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya vyombo vya habari huko Ukanda wa Gaza. taarifa hiyo imeongeza kuwa miili hiyo iliyotolewa katika kaburi la umati imekutwa bila ya vichwa.

Ofisi ya serikali ya Gaza jana ilitangaza kuwa timu ya madaktari wao hadi sasa imefukua miili 49 katika kaburi la umati, na kwamba bado wanaendelea kuwasaka wahanga wengine. Duru kutoka Wizara ya Afya ya Gaza imeeleza kuwa ndani ya kaburi hilo la umati katika hospitali ya al Shifa walikuta vichwa visivyo na miili. 

Picha ya video kutoka hospitali hiyo imeonyesha miili isiyopungua 12 iliyofungwa katika mifuko ya plastiki. Motassem Salah Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Dharura katika hospiatli ya al Shifa amesema kuwa hilo ni kaburi la tatu kugunduliwa ndani ya hospitali hiyo huko Ukanda wa Gaza. Amesema, baadhi ya miili imeoza. 

Takriban miili 30 ilifukuliwa kutoka katika makaburi mengine mawili ya umati kwenye ua wa hospitali ya al Shifa mwezi uliopita. Miili isiyopungua 30 ilifukuliwa kutoka katika makaburi mengine mawili katika ua wa hospitali hiyo hiyo mwezi uliopita.

Wanajeshi wa utawala wa Israel waliwauwa mamia ya Wapalestina na kuiacha miili yao kuoza katika mzingiro na mashambulizi ya wiki mbili dhidi ya hospitali ya al Shifa mwezi Machi mwaka huu. 

Shambulio la Wazayuni katika hospitali ya al Shifa 

Hadi sasa makaburi ya umati yasiyopungua saba yamegunduliwa katika hospitali mbalimbali huko Ukanda wa Gaza tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mapema mwezi Oktoba mwaka jana.