May 10, 2024 10:56 UTC
  • Njama za utawala wa Kizayuni za kuzusha mgogoro wa kibinadamu Rafah

Katika kuendeleza jinai zake utawala wa Kizayuni umepanga kuzusha mgogoro wa kibinadamu huko Rafah.

Licha ya kuwepo tahadhari za kieneo na kimataifa, baraza la mawaziri lenye kupenda vita la utawala haramu wa Kizayuni limezidisha mashambulizi yake dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza, na Washington inaendelea kutoa uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kwa Tel Aviv.

Duru za habari za Palestina zimetangaza kuwa, jeshi la Israel limegeuza Rafah kuwa eneo la kijeshi lililofungwa na linafanya mauaji ya kimbari katika eneo hilo. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka pia limetahadharisha katika ripoti yake kwamba, hali ya upatikanaji wa maji, chakula na dawa huko Gaza imefikia hatua ya hatari na kufunga kivuko cha Rafah kutafanya hali ya wananchi kuwa mbaya zaidi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) pia limeonya kuhusu kuendelea kusitishwa kwa misaada na mafuta katika Ukanda wa Gaza kupitia Kivuko cha Rafah na kueleza kwamba, kuendelea kwa mchakato huu na kusitishwa kuwasili kwa misaada kutazidisha janga la njaa, hasa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Nao Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetahadharisha kuhusu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya mji wa Rafah na kutangaza kuwa, watoto laki sita katika mji huu hawana sehemu salama ya kukimbilia.

Licha ya indhari za taasisi za kimataifa, utawala wa Kizayuni unaendelea na hatua zake zilizopangwa za kuua watu wasio na ulinzi, na wafuasi wa magharibi wa Tel Aviv wanaunga mkono wahusika wakuu wa maafa ya kibinadamu huko Gaza katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na misaada ya fedha, silaha na propaganda za vyombo vya habari. Jinai za hivi sasa za Wazayuni huko Gaza si suala geni na viongozi wa utawala huo haramu katika kipindi cha nusu karne iliyopita daima wamekuwa wakitumia mauaji ya kimbari ili kufikia malengo yao maovu na yasiyo ya kibinadamu.

Kuizingira Gaza na kuzuia misaada ya kibinadamu isipelekwe kwa wananchi wa eneo hilo, kushambulia miundombinu ya matibabu na hata kambi wanamokusanyika wakimbizi wa Kipalestina kutoka vitani ni sehemu tu ya malengo maovu na sera za mauaji ya kimbari za utawala wa Kizayuni ambazo zinalenga kulisafisha eneo hilo na kuendeleza mauaji ya kimbari. Hata hivyo mara hii viongozi wa utawala huo ghasibu wamekabiliwa na matokeo tofauti ya uhalifu wao.

Mwenendo wa maandamano ya umma na ya vyuo vikuu duniani kote umevuta hisia za walimwengu  kwenye jinai za Wazayuni, na vyombo huru vya habari vimekuwa na nafasi athirifu katika kutangaza ukweli wa vita vya Gaza na hali ya sasa ya Rafah. Uwezekano wa kutolewa hati ya kukamatwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ni natija ya mashinikizo ya maoni ya umma ya walimwengu na mashirika ya kimataifa ili wahalifu na wasababishaji wakuu wa mauaji hayo ya kibinadamu na maafa huko Gaza wanashtakiwa na kuwajibishwa kwa uhalifu wao.

Image Caption

 

Sera za kupenda vita Netanyahu na baraza lake la mawaziri zilishika kasi huko Gaza baada ya operesheni ya kimbunga cha Al-Aqswa tarehe 7 Oktoba 2023 na kushindwa jeshi la Kizayuni kukabiliana na makundi ya muqawama huko Palestina.

Wajuzi wa mambo wanaamini kwamba, sera na siasa hizo zimeifanya hali ya uchumi kuwa mbaya na kuibua mgogoro wa kisiasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na kumfanya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na baraza lake la mawaziri kukalia kuti kavu huku mashinikizo ya kujiuzulu yakizidi kuongezeka siku baada ya siku.

Tags