Jumamosi, 11 Mei, 2024
Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria mwafaka na tarehe 11 Mei 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1134 iliyopita, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokezi wa Hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya 4 Hijria. Ibn Khuzaima alianza kutafuta elimu katika miji na nchi mbalimbali akiwa bado kijana. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha al Tauhid wa Ithbat Sifatu al-Rab. ***
Katika siku kama ya leo miaka 328 iliyopita, yaani tarehe 11 Mei mwaka 1696, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa. ***
Tarehe kama ya leo miaka 160 iliyopita alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21 Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960. ***
Miaka 157 iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867, iliundwa nchi ya Magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo imezungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa. ***
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa mwasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989. ***
Katika siku kama leo miaka 89 iliyopita kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho cha kwanza cha matangazo ya televisheni kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha. ***
Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya pamoja ya Ufaransa na Uingereza yaliwasili nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. Hatua hiyo ya Ufaransa na Uingereza ya kuiunga mkono Ubelgiji ilikuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwako baina ya nchi hizo. Licha ya kuweko muungano huo wa kijeshi, vikosi vya Ujerumani ya Kinazi mbali na kuyashinda majeshi ya Ubelgiji vilivishinda pia vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi hiyo. ***
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilijitenga na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo. ***