Apr 28, 2024 07:19 UTC
  • Sudan yataka kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kujadili uchokozi wa Imarati

Sudan imetoa mwito wa kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kile ilichokitaja kuwa uchokozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Sudan inaituhumu Imarati kwamba, inasaidia wanamgambo wanaopambana na jeshi, chanzo cha kidiplomasia kilisema Jumamosi.

Taarifa ya serikali ya Sudan imesema, "jana, mwakilishi wetu wa kudumu katika Umoja wa Mataifa aliwasilisha ombi la kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kujadili uvamizi wa Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya watu wa Sudan, na utoaji wa silaha na vifaa kwa wanamgambo wa kigaidi.

Shirika rasmi la habari la nchi hiyo SUNA limethibitisha kuwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Sudan, Al-Harith Idriss, ndiye aliyewasilisha ombi hilo.

Mohammed Hamdan Dagalo, kiongozi wa kikosi cha Usaidizi wa Haraka Sudan (RSF

 

Majeshi ya Sudan ya Jenerali al-Burhan yanaishutumu Abu Dhabi kwa kusambaza silaha na vifaa, kupitia Chad, kwa wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo ambaye wamekuwa wakipigana naye kwa mwaka mmoja. Hii inawafanya kuhusika katika uhalifu unaofanywa na wanamgambo hao, ameongeza mwakilishi wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa katika harakati zake.

Miezi minane iliyopita, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa, silaha ziligunduliwa katika ndege ya mizigo ya Imarati iliyopaswa kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Sudan nchini Chad.

Hata hivyo Imarati imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na kueleza kwamba, hazina msingi. Aidha serikalii ya Chad nayo imekanusha ripoti hizi. Rais wa mpito wa Chad Mahamat Idriss Déby alisema tena wiki iliyopita kwamba, huo ni uongo.