Ulimwengu wa Spoti, Mei 13
Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia...
Ligi ya Almasi; Wairani watunukiwa
Wanariadha wa Iran wamezoa medali za dhahabu na fedha katika mashindano ya Ligi ya Almasi huko Doha, mji mkuu wa Qatar. Sobhan Ahmadi aliibuka kidedea katika mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume kwa kutumia dakika 1, sekunde 49.98 na kutwaa medali ya dhahabu. Mqatari Zakaria Elhalaami almaliza wa pili kwa kutumia dakika moja, sekunde 49.98 na kushinda fedha huku medali ya shaba ikimuendea raia wa Iraq, Mezah Nooruldeen Adil aliyemaliza mbio hizo kwa kutumia dakika moja, sekunde 50.17.
Muirani Mehdi Pirjahan kwa upande wake alizawadiwa medali ya fedha kwa kumaliza wa pili katika mbio za mita 400 kuruka viunzi, kwa kutumia sekunde 50.60. Alionyeshwa kivumbi na Mlebanoni Marc Anthony Ibrahim huku Muiraqi akifunga orodha ya tatu kwa bora katika kategoria hiyo. Duru ya 4 kati ya 15 ya Mashindano hayo ya Diamond League inatazamiwa kufanyika Rabat, Morocco mnamo Mei 19.
Wakati huo huo, Rais Ebrahim Raisi wa Iran Jumanne iliyopita aliwapokea na kuwaenzi washindi wa Kiirani wa medali tofauti wa mashindano ya olimpiki, paralimpiki, ubingwa wa Asia na ubingwa wa dunia.
Riadha: Kenya yawika Diamond League
Bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola, mbio za mita 800, Mary Moraa kutoka Kenya ametwaa taji la riadha za Ligi ya Almasi (Diamond League) duru ya Doha nchini Qatar. Moraa, ambaye ni bingwa wa mbio za mita 400 na 800, alinyakua taji la Doha katika ziara yake ya kwanza baada ya kukamilisha mizunguko hiyo miwili kwa dakika moja na sekunde 57.96. Aidha Brian Komen, alimzima Mkenya mwenza, bingwa wa dunia, Timothy Cheruiyot katika mbio za mita 1500 kwenye mashindano hayo ya Diamond League mjini Doha.
Kadhalika Beatrice Chebet, alihifadhi taji lake kwenye mashindano hayo katika mbio za mita 5000 kwa upande wa wanawake Ijumaa usiku. Aliwabwaga Wahabeshi Ejgayehu Taye na Eisa Medina. Na nikudokeza tu kuwa, wanariadha wa Kenya, mbali na kutwaa medali kochokocho huko Doha, lakini pia walishinda kategoria zote sita za Mashindano ya Ubingwa wa Dunia ya Mbio za Nyika za Shule jijini Nairobi Jumapili, na kwa mara nyingine tena kudhihirisha kuwa, mbio za masafa za marefu zilizaliwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Dondoo za Hapa na Pale
Tuanze na Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, ambapo ndani ya siku chache zijazo, tujajua ni nani dume kwenye EPL, ni Arsenal au Manchester City. Bila shaka kwa namna mambo yalivyo sasa, matumaini ya Liverpool kutwaa ubingwa ni finyu mno. Arsenal siku ya Jumapili ilirejea kileleani mwa jedwali la EPL baada ya kuibamiza Manchester United bao moja bila jibu, licha ya kuupigia ugenini Old Trafford. Ulikuwa mchuano mgumu na muhimu sana kwa Gunners, na ndiposa wakacheza kufa kupona. Bao la pekee na la ushindi la Wabeba Bunduki katika mechi hiyo lilifungwa na Leandro Trossard kunako dakika 20 ya mchezo, na kuwafanya Mashetani Wekundu waondoke uwanjani wakiwa wameufyata mkia. Kwa ushindi huo, Arsenali imefikisha alama 86, alama moja zaidi, mbele ya mahasimu wao City, ambayo wikendi iliibamiza Fulham mabao 4-0. Josko Gvardiol alifunga mawili kwenye mchuano huo, Phil Fodden akiongeza la tatu, kabla ya Julian Alvarez kulizamisha kabisa jahazi la Fulham kupitia mkwaju wa penati katika dakika za majeraha. Wabeba Bunduki watalazimika kukesha kwa wapiga ramli naona, ili mambo yaitumbukie nyongo City watakapovaana na Tottenham. Mchuano huu, na ule wa Gunners Jumapili ijayo dhidi ya Everton ndiyo itakayoamua nani zaidi kwenye EPL msimu huu, mbali na kutazamwa pia wingi wa magoli. Liverpool kwa sasa anachekea katika nafasi ya tatu akiwa na alama 78.
Katika Ligi ya Klabu Bigwa Barani Ulaya, klabu ya Real Madrid ilihitaji dakika mbili pekee kuizamisha Bayern Munich kwa mabao 2-1 katika mchuano wa nusu fainali ya UEFA Champions League usiku wa kuamkia Alkhamisi. Ilielekea kuwa Munich wangeshinda mechi hiyo na kufuzu fainali, lakini shinikizo la Madrid ambayo ndiyo klabu iliyopata mafanikio makubwa zaidi kwenye mashindano hayo, lilikuwa kubwa mno na likawazidi kete Bayern. Madrid walibebwa na magoli ya Jose Luis Mato Sanmartin (Joselu) katika kipindi cha lala salama. Sasa Madrid itakutana na Borussia Dortmund katika fainali ya dimba hilo. Dortmund tayari ilikuwa imetangulia Madrid, baada ya kuichabanga PSG kwa ujumla wa magoli 2-0 Jumanne.
Na mchezaji nyota wa PSG ya Ufaransa, Kylian Mbappe, ametangaza rasmi kuondoka katika klabu hiyo baada ya kuhumudu ndani ya klabu hiyo kwa miaka saba. Mbappe ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia Mwaka 2018 ametangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo amesema ni mwaka wake wa mwisho PSG na hataongeza mkataba kwenye klabu hiyo. Mechi ya Jumapili Mei 12, dhidi ya Toulouse ndio ilikuwa mechi yake ya mwisho akiwa mchezaji wa PSG.
Ni zaidi ya misimu miwili sasa Mbappe amekuwa akihusishwa na kujiunga na Real Madrid lakini kila dirisha la usajili linapofunguliwa, juhudi za Madrid kumsajili huwa zinagonga mwamba. Mbappe akiwa na PSG, amecheza michezo 306, amefunga mabao 255, na pasi za mabao 108.
………………..MWISHO………….