Upinzani Tunisia wataka dhamana ya uchaguzi huru na wa haki wa rais
Wafuasi wa chama cha Salvation Front wanaompinga Rais Kais Saied wa Tunisia, waliandamana jana Jumapili katikati mwa mji mkuu, Tunis, wakitaka kusafishwa mazingira na hali ya kisiasa, kupangwa tarehe ya uchaguzi wa rais, na kutoa dhamana ya uchaguzi wa kidemokrasia na wa haki kwa wananchi.
Waandamanaji hao walitoa kaulimbiu za kutaka Rais Kais Saied aondolewe madarakani, wakilaani kile walichosema ni utawala wa kipolisi. Vilevile wamelaani kuswekwa jela wapinzani wa serikali ya sasa.
Waandamanaji hao pia walibeba picha za wafungwa wa kisiasa ambao wako jela tangu Februari 2023 kwa tuhuma za "kula njama dhidi ya usalama wa nchi".
Kiongozi wa chama cha Salvation Front, Ahmed Najib Chebbi, amesema kwamba maandamano hayo yanalenga kuishinikiza serikali iache ukandamizaji dhidi ya wapinzani na kutoa dhamana ya kidemokrasia ya uchaguzi huru na wa haki.
Najib Chebbi anasema hali ya sasa ya kisiasa nchini Tunisia haitoi dhamana ya mazingira ya kidemokrasia ya kufanyika uchaguzi wa haki kutokana na kutupwa gerezani wapinzani kwa tuhuma nzito bila ushahidi, kushambuliwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa mahakama na kadhalika.