Apr 27, 2024 08:20 UTC
  • Yemen yashambulia Meli za Uingereza katika Bahari Nyekundu

Shirika la Operesheni za Baharini la Uingereza (UKMTO) lilitangaza jana Ijumaa, kwamba meli yake karibu na pwani ya Yemen imelengwa na kuharibiwa kwa takribani makombora mawili.

Shirika la habari la Iran limesema kuwa:  Shirika la Operesheni za Baharini la Uingereza (UKMTO), ambalo linatazamiwa  kuwa wakala wa usalama, limetangaza kuwa tukio hilo limetokea karibu na pwani ya bandari ya Mokha nchini Yemen, na hakuna aliyetangaza kuhusika  na shambulio hilo wala uharibifu uliotokea.

Kabla ya hapo, kampuni ya usalama ya baharini ya Uingereza Ambri ilitoa ripoti kwamba
shambulio hilo limefanyika kwenye pwani ya Mokha huko Yemen.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, katika kuwaunga mkono watu wa ukanda wa Gaza, wanaharakati  na wapiganaji wa Yemen wamelenga meli kadhaa za utawala haramu wa Kizayuni au zinazobeba mizigo kwa ajili ya utawala huo zilizokuwa zikienda katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko Palestina, katika Bahari Nyekundu, Bahari ya Hindi na mlango bahari wa Bab al-Mandab.

Vikosi vya wanaharakati na wapiganaji wa Yemen vimeahidi kuwa  vitaendelea kuzishambulia meli za utawala haramu wa Israeli, na vikosi vinavyounga mkono utawala huo haramu wa Kizayuni, au meli zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu huko Palestina, katika Bahari Nyekundu, hadi pale utawala huo bandia wa Israel utakapoacha na kusimamisha mashambulizi yake dhidi ya watu wanaodhulumiwa huko Gaza.