May 09, 2024 07:21 UTC
  • MSF: Kufunga kivuko cha Rafah kutaifanya hali ya Gaza kuwa mbaya zaidi

Mkuu wa timu ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ametahadharisha kuwa mazingira ya kuidhaminia Gaza maji safi, chakula na dawa za matibabu yamefika marhala hatari na kwamba hatua ya kukifunga kivuko cha Rafah kunaifanya hali ya wakazi wa ukanda huo kuwa mbaya zaidi.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Aurélie Godard Mkuu wa timu ya Madaktari Wasio na Mipaka huko Gaza ametaka kufunguliwa kivuko cha Rafah na kusema misaada ya kibinadamu, vifaa tiba, chakula na fueli haviwezi tena kuingizwa Ukanda wa Gaza. 

Godard ametahadharisha kuhusu kupungua pakubwa huko Gaza maji safi, chakula na dawa za matibabu na kuongeza kuwa: Baada ya kupita miezi saba ya vita ambavyo vimesababisha watu milioni moja na laki saba kuhama makazi yao; uamuzi wa kukifunga kivuko cha Rafah utazidisha tu hali mbaya kwa wakazi wa Gaza. 

Aurelie Godard, Mkuu wa MSF Ukanda wa Gaza

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametahadharisha kuwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika mji wa Rafah yatasababisha maafa ya binadamu na kuyataja kuwa ni kosa la kistratejia. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni na harakati ya Hamas kufikia makubaliano ya usitishaji vita na kuzuia uvamizi kamili wa utawala huo mjini Rafah. 

Siku ya Jumatatu (tarehe 6 Mei), baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni liliidhinisha shambulio la ardhini dhidi ya mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza licha ya upinzani wa kimataifa. Jeshi la utawala wa Israel limekalia kwa mabavu sehemu ya kivuko cha Rafah mashariki mwa mji huo tangu juzi Jumanne. 

Tags