Mar 10, 2024 11:20 UTC
  • Kukosolewa propaganda za Marekani kuhusiana na misaada ya kibinadamu

Akihutubia bunge la Marekani siku ya Alkhamisi, Rais Joe Biden alisema ameliamuru jeshi la nchi hiyo kuweka bandari kwenye pwani ya Gaza katika Bahari ya Mediterania.

"Gati ya muda itawezesha kuwepo ongezeko kubwa la misaada ya kibinadamu inayoingia Ghaza," alisema Biden katika hotuba yake hiyo.

Katika mwezi wa sita wa vita vya Gaza na kuendelea mauaji ya kimbari ya watu madhulumu wa Ukanda wa Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani ambayo ni mshirika wa jinai za utawala huo ghasibu, katika radiamali yake kwa kuongezeka ukosoaji wa ndani na wa kimataifa kutokana na himaya kubwa ya kisiasa na kijeshi kwa Tel Aviv, inaonekana imeamua kuanzisha propaganda ambazo kidhahiri zinaonekana ni kwa ajili ya kuwasaidia wakaazi wa Gaza. Hata hivyo hatua hizo zimekabiliwa na ukosoaji mwingi.

Avril Benoit, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) sambamba na kuaashiria mpango wa Marekani wa kujenga gati ya muda huko Gaza kwa kisingizio kuwezesha kuingizwa misaada katika Ukanda wa Gaza amesema,  kwa hatua hii Washington inataka kuwapotosha walimwengu kuhusiana na matatizo halisi ya Ukanda wa Gaza ambayo ni hujuma na mashambulio ya kinyama ya wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya Gaza na mzingiro wa kuwaadhibu raia wa Palestina katika eneo hilo.

Wakaziu wa Gaza wakisubiria chakula cha msaada

 

Akieleza kuwa hali ya sasa ya Gaza ni matokeo ya tatizo la kisiasa na si tatizo la vifaa amedokeza kuwa, badala ya kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa gati hiyo, Marekani inapaswa kusisitiza kupelekwa misaada ya kibinadamu kupitia njia zilizopo. Avril Benoit ameongeza kusema kuwa, kusitishwa kwa mapigano ni njia pekee ya dhamana ya kweli ya kupelekwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Ukosoaji mkali wa Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) dhidi mpango mpya wa Washington kwa kisingizio cha kuisaidia Gaza hauna maana yoyote hasa kwa kuzingatia utendaji wa kinafiki na kindumakuwili wa Marekani kuhusiana na vita vya Gaza. Kwa upande mmoja, serikali ya Biden imetoa uungaji mkono mkubwa na  usio na kikomo kwa utawala wa Kizayuni, ambapo sambamba na kupinga kwa kutumia kura ya veto maazimio yote ya Baraza la Usalama yaliyotaka kusimamisha vita vya Gaza, imekuwa ikitoa silaha kikamilifu kwa utawala huo.

Kwa hakika Washington haijawahi kuweka shinikizo kubwa kwa Israel, na serikali ya Biden hadi sasa haijachunguza machaguo kama vile kuiwekea vikwazo Israel au kuwekea masharti mabilioni ya dola za msaada wa kijeshi. Wakati huo huo ripoti mpya zinaonyesha kuwa, mbali misaada rasmi ya silaha ya serikali ya Biden kwa Tel Aviv, Marekani imetuma pia shehena 100 za silaha kwa siri huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kwa upande mwingine, badala ya serikali ya Biden kuweka mashinikizo ya kweli na sio tu ukosoaji wa wazi dhidi ya Israe wa wa usitishaji vita Gaza na kufanya juhudi kubwa kufungua njia zilizopo, ukiwemo mpaka wa Rafah, ambapo idadi kubwa ya malori ya kubeba vyakula na vitu vya msingi yanasubiri kuingia Gaza, imechukua hatua kama vile mpango wa kujenga gati huko Gaza.

 

Kadhalika kufuatia kushadidi mashinikizo dhidi ya serikali ya Biden kutokana na uungaji mkono wake kwa Israel, na Tel Aviv kutumia njaa ya watu wa Gaza kama wenzo wa mashinikizo, Marekani licha ya kuunga mkono utawala huo, imeanzisha onyesho la propaganda sambamba na kukaribia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, ambapo imetumia ndege zake za usafiri wa jeshi kwa ajili ya kusafirisha chakula na vifaa vingine hadi Gaza kama ufumbuzi wa upinzani wa Israel wa kupelekwa misaada katika Ukanda wa Gaza na kuwafikia wahitaji misaada hiyo.

Maafisa wa mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada wanachukulia hatua hii ya Marekani kuwa isiyofaa na lengo lake ni kujipigia debe.

Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula, Michael Fakhri amepuuzilia mbali mpango wa Rais wa Marekani wa kuanzisha bandari inayodaiwa kuwa na lengo la kuwezesha kuingizwa misaada katika Ukanda wa Gaza, ulioteketezwa kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vikiungwa mkono kwa hali na mali na serikali ya Washington.  Hatua hiyo anayokusudia kuchukua rais wa Marekani ni ya jaribio la kuvutia uungaji mkono ndani ya nchi hiyo wakati uchaguzi wa rais ukiwa unakaribia. Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ametamka bayana kuwa, si gati wala si matone ya misaada iliyodondoshwa na Marekani hivi karibuni huko Gaza, ambayo Wapalestina na waungaji mkono wao wameyadhihaki kuwa ni ya kimaonyesho tu, yatazuia njaa na dhiki ya chakula kwa tafsiri yoyote ile. Wakati huo huo, Wapalestina watano wameuawa kwa vifurushi vya misaada vilivyodondoshwa na ndege za Marekani na washirika wake kwenye Ukanda wa Gaza unaozingirwa na Israel, huku mamlaka ya Gaza ikilishutumu zoezi hilo kuwa ni "propaganda tupu" na sio huduma ya kibinadamu. Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha ndege ikidondosha vifurushi vya msaada kwa watu katika Kambi ya al-Shati kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Wenyeji wanasema miavuli iliyotumika kudondosha misaada haikufunguka, na kusababisha masanduku kuwaangukia watu wanaohitaji sana msaada ya chakula, maji na dawa.

Mashambulio ya anga ya Israel yalivyoharibu Gaza

 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hatua hizo za Marekani zinafanywa kwa ajili tu ya kupunguza mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Ikulu ya White House kutokana na nafasi yake madhubuti katika kuendeleza jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Hii ni katika hali ambayo, hali ya Gaza imevuka mpaka wa maafa, na Tel Aviv imeingia vitani na watu wanaodhulumiwa kwa silaha ya njaa na Ukanda wa Gaza uko kwenye hatihati ya kuingia katika hatua mbaya ya njaa.

Hapana shaka kuwa, kuendelea mwelekeo na utendaji wa sasa wa Ikulu ya White House kuhusiana na vita vya Gaza na uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni kutapunguza kura za Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa Marekani kutoka kwa wafuasi kindakindaki wa Chama cha Kidemokrasia na kuongeza uwezekano wa kushindwa mwanasiasa huyu anayekabiliwa pia na matatizo ya udhaifu wa kukumbuka mambo.

Tags