May 08, 2024 05:52 UTC
  • Utawala wa Israel wawazuia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuingia Rafah

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu amesema kuwa, utawala wa Kizayuni unawazuia wafanyakazi wa umoja huo kuingia katika kivuko cha Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Askari wa utawala wa Kizayuni wakiingia Rafah

Jens Lairke, Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu alisema jana usiku mjini Geneva huko Uswisi kwamba wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hawapo tena  katika  maeneo ya kivuko cha Rafah kutokana na vizuizi vilivyowekwa na utawala haramu wa Israeli katika mji huo kusini mwa ukanda wa Gaza.

Jens Lairke ameongeza kwa kusema kwamba: Hivi sasa haiwezekani kabisa watu au bidhaa kuingia na kutoka katika kivuko cha Rafah huko ukanda wa Gaza na hili lina taathira na madhara makubwa kwa juhudi za misaada ya kibinadamu inayotolewa na Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza.

Kivuko cha Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza ndicho kivuko kikuu cha misaada ya kibinadamu inayoingia Ukanda wa Gaza kwa ajili ya kusaidia watu madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina wanaokandamizwa na utawala ghasibu wa Israeli.

Utawala wa Kizayuni unaendelea kushambulia maeneo ya mashariki ya mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza tokea jana Jumanne asubuhi.

Makumi ya watu wameuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi hayo yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israeli, ambapo wanawake na watoto ni miongoni mwa mashahidi na majeruhi.

Duru za Palestina zinasema kuwa, mashambulio hayo makali ya utawala ghasibu wa Israel katika mji wa Rafah yangali yanaendelea ambapo utawala ghasibu wa Israel umeugeuza mji huo kuwa eneo la kijeshi na uwanja wa vita kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa eneo hilo.