May 07, 2024 11:32 UTC
  • Mataifa ya Afrika Mashariki yaazimia kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR

Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini zimeazimia kuweka nguvu ya pamoja ili kufanikisha ujenzi wa reli ya mwendo kasi (SGR) inayopita Afrika Mashariki.

Mawaziri wa usafiri na uchukuzi kutoka mataifa hayo wamekubaliana kwa pamoja kutafuta wafadhili na wajenzi wa reli hiyo, kurekebisha mkataba wa maelewano na kuhusisha mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini na vile vile jinsi ya kugawana majukumu ya kulinda reli hiyo ya SGR.

Waziri wa uchukuzi wa Uganda Fred Byamukama amesema, wamechukua mkondo huu kupunguza gharama ya kufanya biashara kuimarisha uchukuzi na kuunganisha mataifa hayo na pia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Uganda imefikia hatua za mwisho za mkataba kati ya wafadhili kufanya ujenzi wa SGR kutoka Mpakani Malaba hadi mji mkuu Kampala.

Naye Kipchumba Murkomen Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya amebainisha kwamba, nchi yake itarejea katika ujenzi wa reli ya SGR kutoka Naivasha kwenda mpakani Malaba mwaka huu kwa gharama ya dola bilioni 5.3 ambazo inakusudia kupata kutoka sekta binafsi.

Kipchumba Murkomen Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya

 

Ujenzi wa SGR Afrika Mashariki umegawanywa kwa vipande, kutoka Naivasha mpaka Malaba kisha Uganda itaunganisha Malaba na Kampala, sehemu ya tatu ni kati ya Kampala, Bihanga Kasese - Mpondwe mpaka DR Congo sehemu ya nne ikiwa kati ya Bihanga mpaka Milima ya Mirama na kisha mji mkuu Kigali Rwanda, sehemu ya tano ni kati ya Tororo – Gulu, mpaka Sudan Kusini Pakwach na Vurra.

Rwanda inapojiunga na msukumo huu waziri wa uchukuzi Jimmy Gasore amesisitiza umuhimu wa ushirikiano ambao utaharakisha na kupunguza mzigo wa kujenga reli ya SGR na hivyo kuwa ya faida kwa mataifa hayo.