May 19, 2024 10:42 UTC
  • Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Afghanistan yafikia watu 400

Idadi ya vifo vilivyosababishwa na mvua kubwa na mafuriko yaliyoikumba Afghanistan imefikia 400 baada ya watu wengine 18 kufariki dunia kutokana na mafuriko hayo.

Msemaji wa jimbo la Faryab Ismetullah Muradi amevieleza vyombo vya habari kuwa watu wasiopungua 18 wamepoteza maisha katika mafuriko yaliyotokea katika jimbo hilo lililoko kwenye mpaka wa pamoja na Turkmenistan na kuifanya idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo katika wiki za hivi karibuni kufikia 400.
 
Muradi amebainisha pia kuwa zaidi ya hekta 2,000 za ardhi ya kilimo zimeharibika, nyumba 1,000 zimebomoka na zaidi ya wanyama 300 wamekufa.

Watu wapatao 50 wamepoteza maisha na makumi ya wengine hawajulikani waliko kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyolikumba a jimbo la Ghor.

 
Mafuriko makubwa yaliyotokea wiki iliyopita kaskazini mwa Afghanistan, hususan katika majimbo ya Baghlan, Badakhshan, na Takhar, yamesababisha hasara, maafa  na uharibifu mkubwa.
 
Kuyeyuka theluji wakati wa miezi ya baridi nchini Afghanistan kutokana na kuongezeka kwa joto kunakochanganyika na mvua kubwa na kuwepo kwa miundombinu dhaifu, husababisha mafuriko yanayopelekea kutokea hasara na maafa makubwa ya mali na roho za watu. Mamia ya watu hufariki dunia kila mwaka nchini humo kutokana na majanga hayo.../

 

Tags