Apr 28, 2024 11:47 UTC
  • Mkuu wa UNRWA atahadharisha: Israel inajiandaa kufanya shambulio kubwa la kijeshi Rafah

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA amesema, utawala wa Kizayuni unajiandaa kwa operesheni kubwa ya kijeshi katika mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Ghaza.

Philip Lazzarini ameeleza kuwa ana wasiwasi kuhusu mashambulizi makubwa yanayopangwa kufanywa na jeshi la utawala wa Israel dhidi ya mji wa Rafah na akaongeza kuwa zaidi ya Wapalestina milioni moja na laki nne na nusu waliobaki bila makazi, hivi sasa wamerundikana kusini mwa Ghaza na nchi zote duniani zimeshatangaza kuwa shambulio hilo halipasi kufanywa kwa namna yoyote ile.
 
Lazzarini ametamka bayana kuwa operesheni ya kuivamia kijeshi Rafah kupitia nchi kavu "inatia wasiwasi mno" na akaongeza kuwa kwa vile hakuna mahala popote penye usalama katika Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya makazi, watu wana hofu kubwa kwa sababu hawajui wapi pa kwenda.
Rafah, walikorundikana Wapalestina wapatao milioni moja na nusu

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina amesisitiza kuwa, hakuna shaka yoyote kwamba maelfu ya watu watauawa iwapo litafanywa shambulio dhidi ya mji wa Rafah.

 
Lazzarini amedokeza kuwa baadhi ya nchi zinataka kuivunja UNRWA kwa sababu za kisiasa ili kudhoofisha juhudi za kuundwa taifa la Palestina na akaongeza kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kupinga na kukabiliana na hatua hiyo.
UNRWA ndilo shirika kubwa zaidi la utoaji misaada katika Ukanda wa Ghaza.
 
Wafanyakazi wapatao elfu kumi na tatu wa shirika hilo walikuwa wakifanya kazi wakati wa vita, na kwa sasa elfu tatu kati yao wanaendelea kuhudumu katika shirika hilo.
 
Mbali na usambazaji wa chakula, UNRWA inatoa elimu na huduma za msingi za matibabu katika Ukanda wa Ghaza.../

 

Tags