Iran: Kuipa uanachama Palestina, ni hatua ya kwanza ya kukabiliana na dhulma
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Tehran inakaribisha hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA ya kupasisha azimio la kutaka kutazamwa upya suala la taifa la Palestina kupewa uanachama kamili katika umoja huo.
Amir Saeid Iravani amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha na inaunga mkono kikamilifu suala la Palestina kupewa uanachama kamilii katika Umoja wa Mataifa.
Ameeleza bayana kuwa, kupewa Palestina uanachama kamili ndani ya Umoja wa Mataifa ni hatua ya kwanza ya kukabiliana na dhulma za kihistoria dhidi ya taifa hilo, na kufidia madhila waliyoyapitia Wapalestina.
Azimio hilo lililowasilishwa na Imarati kwa niaba ya madola ya Kiarabu, lilipitishwa jana Ijumaa kwa kura 143 za kuunga mkono, 9 zinazopinga, na 25 za nchi ambazo zimejizuia kupiga kura.
Licha ya azimio hilo kuliongezea taifa la Palestina haki ndani ya Baraza hilo, lakini bado nchi hiyo ya Kiarabu haitakuwa na haki ya kupiga kura ndani ya chombo hicho cha ngazi ya juu cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, Tehran inakaribisha uamuzi huo wa Baraza Kuu la UN wa kupasisha azimio linalosisitiza kuwa Palestina imetimiza vigezo vya kupewa uanachama kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Hati ya UN.
Mwanadipomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, ingawaje hatua hiyo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni ndogo, lakini ni muhimu katika mchakato wa jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake kwa Wapalestina, na kuhuisha baadhi ya haki za msingi za wananchi hao madhulumu.