Apr 27, 2024 08:11 UTC
  • Iran kuimarisha uhusiano wa kijeshi na Russia, China

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigadier Jenerali Mohammad Reza Ashtiani amekutana na mawaziri wenzake wa ulinzi wa China na Russia kujadili njia za kuimarisha zaidi uhusiano wa kijeshi kwa ajili ya kuimarisha usalama na uthabiti duniani.

Jenerali Ashtiani amefanya mazungumzo hayo kando ya mkutano wa 21 wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) uliofanyika Ijumaa huko Astana, Kazakhstan.

Katika mazungumzo na mwenzake wa China Jenerali Dong Jun, Ashtiani alipongeza msimamo wa China kuhusu  matukio yanayoendelea katika eneo hasa kulaani mashambulizi ya anga ya kigaidi ya Israel dhidi ya eneo la ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus mapema mwezi huu.

Waziri wa ulinzi wa China kwa upande wake amelaani tena shambulizi la Israel dhidi jengo la kidiplomasia la Iran nchini Syria, ambalo alisema linakiuka sheria za kimataifa. Aidha amesema China inaunga mkono haki halali ya Iran kulipiza kisasi hujuma hiyo ya Israel. Dong amemwalika mwenzake wa Iran kushiriki katika mkutano wa usalama mjini Beijing na kuhimiza kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za ulinzi na kijeshi.

Wakati huo huo, katika mkutano na Waziri wa Ulinzi wa Russia, Jenerali Sergei Shoigu, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Tehran na Moscow zinapaswa kupinga sera ya kuchukua maamuzi ya upande mmoja katika masuala ya kimataifa.

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani (wa tatu kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Russia  Jenerali Sergei Shoigu (wa tatu kutoka kushoto) mjini Astana, Kazakhstan, Aprili 26, 2024. (Picha imesambazwa na Wizara ya Ulinzi ya Iran)

Ameishukuru Russia kwa kulaani mashambulizi haramu ya anga yaliyotekelezwa na Israel dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus na hatua ya Moscow ya kuunga mkono jibu halali la Tehran. Ashtiani aidha amesema mashambulizi ya kigaidi  huko Russia na pia nchini Iran ni matokeo ya uungaji mkono wa nchi za Magharibi, hasa Marekani, kwa makundi ya kigaidi.

Katika kikao hicho Waziri wa Ulinzi wa Russia amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran mjini Damascus na kusema hatua ya Iran ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel ilikuwa kwa mujibu wa haki halali ya kujilinda.

Ashtiani na Shoigu pia wamesisitiza kuhusu ushirikiano wa nchi mbili ili kukabiliana na vitisho vya kigaidi, wanaotaka kujitenga na wenye misimamo mikali.