May 09, 2024 13:03 UTC
  • HRW: Kuna uwezekano RSF wamefanya mauaji ya halaiki Sudan

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema kuwa, mfululizo wa mashambulizi ya vikosi vya wanamgambo vya Sudan katika eneo la Darfur unaongeza uwezekano wa "mauaji ya halaiki".

Hayo yamo katika ripoti ya Human Rights Watch ambayo imetahadharisha kuhusiana na hujuma na mashambulio ya kikosi hicho kinachoongozwa na jenerali Hamdan Dagalo.

Wanasheria wa haki za binadamu katika maeneo hayo wameelezea kufuatilia namna ambapo wapiganaji walilenga "wanachama mashuhuri wa jumuiya ya Massalit", wakiwemo madaktari, watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa eneo hilo na maafisa wa serikali.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) inaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

 

Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba.

Hivi karibuni Justin Brady, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini Sudan alisema, "leo, Sudan ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Nusu ya wakazi wa Sudan yaani watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu."