May 09, 2024 12:18 UTC
  • Iran yataka Umoja wa Mataifa uishinikize zaidi Israel inayofanya mauaji ya kimbari

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametahadharisha dhidi ya kuendelea utendaji hatari wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kutaka kuongezwa mashinikizo hususan kutoka Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala huo ghasibu.

Hussein Amir-Abdollahian Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambapo amepongeza juhudi za Katibu Mkuu za kukomesha vita na mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea na juhudi za kurejesha usalama na uthabiti katika eneo hili hususan kuhitimisha jinai za utawala ghasibu wa Israel.

Amir Abdollahian ameonya kwamba iwapo Marekani, badala ya kumshinikiza Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel akubali kusitishwa mapigano, itaudekeza utawala huo katika kufanya jinai mpya huko Rafah, matokeo mabaya yatakuwa makubwa kwa waungaji mkono wa vita hivyo.

Athari ya mashambulio ya kijeshi ya Israel katika mji wa Rafah

 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran sambamba na kutangaza kuunga mkono jibu la Hamas kwa mpango wa kusimamisha vita amesema kuwa, utawala wa Kizayuni katika kuendeleza "sera yake ya ugaidi na mauaji ya kimbari" sasa unafanya njama za kuibua maafa mengine ya kibinadamu katika eneo hilo kwa kufunga kivuko cha Rafah na Karem Abu Salem na hivyo kukwamisha juhudi za kimataifa za kukomesha vita.