Apr 27, 2024 12:32 UTC
  • Kindiki: Daktari gaidi atumikie kifungo cha miaka 12 kwa kupanga kuangamiza Wakenya

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amekataa jaribio la kupunguza kifungo cha miaka 12 jela dhidi ya gaidi aliyepanga kuangamiza Wakenya akitumia sumu ya kemikali ya virusi vya ugonjwa wa kimeta (Anthrax).

Prof Kindiki ameamuru Dkt Mohamed Abdi Ali aliyefungwa na hakimu mkuu Martha Mutuku atumike kifungo chote.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya amekataa kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha Sheria nambari 46 ya Sheria za Magereza kumpunguzia kifungo Dkt Ali aliyepatikana na hatia ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la ISIS.

Kindiki amesema Dkt Ali angali hatari kwa usalama wa umma. Amesema Dkt Ali hakujutia matendo yake na wala hajaonyesha ishara yoyote ya kubadilika.

Dr Mohamed Ali 

Mfungwa huyo alikuwa amepelekwa kuhudumu katika Hospitali ya Makueni Level 4 mjini Wote 2016. Alikamatwa na kushtakiwa kuwa mwanachama wa kundi la ISIS na Al-Shabaab.

Vilevile alipatikana na hatia ya kuwaingiza vijana katika kundi la ISIS. Pia alikuwa anatoa mafunzo ya itikadi kali kwa vijana aliowapeleka kupokea mafunzo nchini Somalia na Libya.

Bi Mutuku alimpata na hatia katika mashtaka matano ya ugaidi na kumsukuma jela miaka 12 kwa kila shtaka.