Uwezekano wa ICC kutoa waranti wa kukamatwa Netanyahu kwa mauaji ya Ghaza umeitia tafrani Israel
Baraza la mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limeingiwa na tafrani na wasi wasi mkubwa juu ya uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu na maafisa wengine waandamizi kwa kuhusika na jinai za vita vya miezi kadhaa vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza uliozingirwa.
Katika siku za hivi karibuni, Netanyahu amewapigia simu viongozi na maafisa wa kimataifa hususan Rais Joe Biden wa Marekani kumtaka azuie kutolewa waranti wa kumkamata.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika kile kinachoonekana kama hatua ya kupinga dhahiri kutolewa kwa hati hiyo inayoripotiwa kuwa yamkini ikatolewa mnamo "siku chache zijazo," waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni alisema Ijumaa kwamba uamuzi wa ICC hautaathiri vita vyake huko Ghaza, ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 34,000.