Apr 28, 2024 10:52 UTC
  • Kushadidi mgogoro wa kisiasa katika baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni

Kuendelea maandamano ya mitaani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), tofauti za kimtazamo kati ya wapinzani na baraza la mawaziri na kuongezeka uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kutoa amri ya kumkamata Benjamin Netanyahu kumezidisha mzozo wa kisiasa huko Tel Aviv.

Matokeo ya oparesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa" iliyoanzishwa na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023, yamezidisha hali ya sintofahamu na ukosefu wa utulivu katika utawala wa Kizayuni, na sasa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu linaelekea kusambaratika.

Katika muktadha huo, Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa serikali ya Israel, Jumamosi ya jana tarehe 27 Aprili alishiriki katika maandamano ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv. Familia za mateka wa Kizayuni na maelfu ya wapinzani wa baraza la mawaziri la Netanyahu pia zilifanya maandamano mbele ya jengo la Wizara ya Vita ya utawala wa Israel huko Tel Aviv. 

Gazeti la Kizayuni la Ma'ariv pia limeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ana wasiwasi mkubwa na amefadhaishwa na hofu ya kutolewa hati ya kukamatwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Gaza

Mgogoro wa kisiasa umeongezeka zaidi huko Tel Aviv katika siku za hivi karibuni, na vyama vya upinzani vimetoa wito wa kufanyika uchaguzi wa mapema na kuondolewa madarakani Benjamin Netanyahu. Maandamano makubwa ya mitaani pia yanafanyika mtawalia katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, na waandamanaji wanamtambua Netanyahu kuwa sababu kuu ya kuendelea vita huko Gaza na kushindwa kufikiwa makubaliano katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na harakati ya Hamas.

Mwanzoni mwa vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza, Benjamin Netanyahu alitoa ahadi kadhaa, lakini baada ya muda, inaonekana wazi kwamba hana uwezo wa kuzitekeleza. Miongoni mwa ahadi hizo ni kuiangamiza harakati ya Hamas na makundi mengine ya ukombozi ya Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Hata hivyo Netanyahu ameshindwa kutekeleza ahadi hiyo, na jeshi la Israel limepata kipigo na kushindwa vibaya na kuishia kuua raia wasio na hatia. 

Kukomboa mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na harakati za mapambano za Palestina pia ilikuwa miongoni mwa ahadi za Netanyahu ambazo bado hazijatimia kutokana na vizingiti vinavyowekwa na wawakilishi wa utawala wa Kizayuni katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na Hamas. Kuendelea vita vya Gaza pia kumeifanya hali ya Israel kuwa ngumu zaidi kiuchumi, na baraza la mawaziri la Netanyahu limeshindwa kudhibiti vita hivyo.

Jinai zinazofanywa na jeshi la Israel na mauaji ya maelfu ya wanawake na watoto wasio na ulinzi huko Gaza pia vimezidisha chuki ya walimwengu kwa utawala wa Kizayuni. Ijapokuwa vyombo vya habari vyenye mfungamano na Marekani na nchi za Magharibi vinachuja sana habari za vita vya Gaza, lakini wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina na makundi ya kutetea amani yameweza kuunda muwafaka wa kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Wakati huo huo, Mahakama ya Kimataifa ya Haki, (ICJ) huenda ikachunguza kadhia ya jinai zinazofanywa na Israel katika siku chache zijazo, na watuhumiwa wakuu wa jinai na mauaji ya kinyama huko Gaza ni Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na wanachama wenye misimamo mikali wa baraza lake la mawaziri. Utawala wa Kizayuni unaandamwa na migogoro mingi ya ndani na wajumbe wa baraza la mawaziri la Netanyahu pia wako katika hatihati ya kufikishwa mahakamani na kufuatiliwa kimataifa.

Maandamano ya Wazayuni Israel

Kwa maelezo haya yote inaonekana kuwa, vita vya Gaza vimegeuka kuwa jinamizi kwa Netanyahu na baraza lake la mawaziri, kiasi kwamba hali ya ndani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu imekuwa mbaya zaidi, na uwezekano wa baraza la mawaziri kuanguka unaongezeka kila siku. Netanyahu pia anatofautiana na Wazayuni wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri, na mivutano hiyo inaongezeka kila uchao. Athari mbaya za ndani na nje za uchochezi wa Israel zimezidisha migogoro ya kisiasa na kiuchumi katika utawala huo ghasibu na kuuweka kwenye ukingo wa kuporomoka. 

Tags