Jan 01, 2024 12:20 UTC
  • Kadhaa wauawa Abyei mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini

Kwa akali watu sita wameuawa katika shambulizi linaloamini ni la ulipizaji kisasi katika eneo linalozozaniwa la Abyei, kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, miongoni mwa watu waliouawa kwenye mapigano hayo 'ya kikabila' ni afisa wa serikali za mitaa katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta. Wakazi wakuu wa eneo hilo ni watu wa kabila la Dinka la Sudan Kusini na kabila la Masiriya la Sudan.

Habari zaidi zinasema kuwa, Naibu Mratibu Mkuu wa Abyei, Noon Deng pamoja na timu yake wameshambuliwa wakiwa barabarani kwenda mji wa Aneet wakitokea Abyei, kaunti ya Rummamer.

Tereza Chol, Mbunge wa Sudan Kusini ameiambia Reauters kuwa, dereva wa afisa huyo wa Abyei, walinzi wake wawili pamoja na maafisa wa usalama wa taifa wameuawa katika shambulizi hilo.

Bulis Koch, Waziri wa Habari wa eneo la kiutawala la Abyei amesema shambulizi hilo la jana usiku limefanywa na vijana kutoka kaunti ya Twic jimbo la Warrap na kwamba maiti za waliouawa zilikuwa katika eneo la tukio mpaka asubihi ya leo Jumatatu.

Mwishoni mwa mwaka uliomalizika, watu 32 waliuawa katika mapigano makali yaliyozuka kwenye eneo hilo linalozozamiwa katika mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.

Abyei imeendelea kuwa eneo lenye mzozo mkubwa kati ya Sudan Kusini na jirani yake Sudan ambayo kwa sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa wa ndani tangu Aprili 15. 

Tags