Apr 27, 2024 02:36 UTC
  • Sanders amwambia Netanyahu: Kusema kwamba umeua watu 34,000 sio chuki dhidi ya Wayahudi

Seneta wa mrengo wa kushoto wa Marekani, Bernie Sanders, amemshambulia vikali Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisisitiza haja ya kutochanganya kauli za kulaani mauaji yanayofanywa na Israel huko Gaza na chuki dhidi ya Wayahudi.

Sanders amemwambia Netanyahu kwamba: "Kusema serikali yako imeua watu 34,000 katika muda wa miezi 6 sio chuki dhidi ya Wayahudi wala sio kuunga mkono harakati ya Hamas."

Seneta huyo wa Marekani ameongeza kuwa, kulaani kitendo cha serikali ya Netanyahu cha kuharibu vyuo vikuu na shule za Gaza na kuwanyima elimu watu 625,000 si chuki dhidi ya Wayahudi.

Bernie Sanders amesema kumwambia Waziri Mkuu wa Israel: "Kusema kwamba umeharibu miundombinu ya Gaza, mfumo wa afya na nyumba 221,000 za raia sio chuki dhidi ya Wayahudi."

Watoto wa Gaza

Siku mbili zilizopita pia, Sanders alisema kwamba kinachofanywa na Israel huko Gaza si vita dhidi ya Hamas, bali ni kuangamiza msingi wa maisha ya Wapalestina.

Sanders ambaye alikuwa akihutubia Bunge la Congress lililokutana kuidhinisha misaada ya kigeni, ikiwa ni pamoja na msaada wa kijeshi kwa Israel, alieleza kwamba kinachotokea Gaza si ajali au makosa ya kivita, bali ni sera iliyopangwa kwa mahesabu ambayo imetekelezwa kwa mpangilio maalumu kwa zaidi ya miezi 6.

Seneta huyo wa Marekani pia amekosoa ushiriki wa serikali ya nchi hiyo katika vita dhidi ya watu wa Gaza na kusema kwamba, vita vya Gaza ni vita vya Israel na Marekani.

Ameeleza kuwa "mabomu mengi na vifaa vya kijeshi vinavyotumiwa na Israel huko Gaza vinatolewa na nchi yetu kwa pesa za walipa kodi za Kimarekani."

Karibu Wapalestina elfu 35 wameuawa hadi sasa na wengine zaidi ya elfu 76 wamejeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza.