May 07, 2024 06:38 UTC
  • Maseneta 12 wa Marekani waitishia ICC: Mkiiandama Israel tutakuandameni

Maseneta 12 wa chama cha Republican nchini Marekani wameitishia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwamba itawekewa vikwazo na Washington endapo itatoa hati za kukamatwa viongozi wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Ghaza.

Barua hiyo ya ukurasa mmoja iliyopatikana na tovuti ya habari ya mtandaoni ya Zeteo, imetumwa kwa Mwendesha Mashtaka wa ICC Karim Khan ikimhutubu ya kwamba "vibali vyovyote vya kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wakuu wa Israel si halali na havina msingi wa kisheria, na endapo vitatekelezwa vitasababisha vikwazo vikali dhidi yako na taasisi yako".
 
"Mkiiandama Israel tutakuandameni," wameeleza maseneta hao 12 wa Marekani katika barua yao hiyo ya vitisho wakiendelea kusema: "ili kuweka wazi ni kwamba, hakuna usawa wa kimaadili kulinganisha ugaidi wa Hamas na jibu halali la Israel".
 
Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na Tom Cotton, Mitch McConnell, Rick Scott, Tim Scott, Ted Cruz, na Marco Rubio.
 
Vikwazo vinavyotishiwa na maseneta hao vitawalenga wafanyakazi wa ICC na washirika wao na vitajumuisha vikwazo vya viza kwa familia za wafanyakazi wa mahakama hiyo.
Chris Van Hollen

Hata hivyo Seneta wa chama cha Democratic Chris Van Hollen amewashutumu maseneta wenzake wa chama cha Republican kwa kujihusisha na alichokiita "ujambazi" dhidi ya mahakama kuu ya kimataifa.

 
"Ni sawa kupinga hatua ambayo yamkini itachukuliwa na mahakama, lakini ni makosa kabisa kuingilia suala la mahakama kwa kuwatishia maafisa wa mahakama, wanafamilia wao na wafanyakazi wao kwa ulipizaji kisasi. Ujambazi huu ni jambo la kufanywa na mafia, si maseneta wa Marekani " ameeleza Seneta Hollen katika taarifa yake kwa Zeteo.
 
Mahakama ya ICC iliyoko The Hague, hivi sasa inafanya uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita unaoripotiwa kufanywa na jeshi la Israel.

Uvumi umeenea kwamba mahakama hiyo inaweza kutoa hati za kukamatwa maafisa wakuu wa Israel kwa kuhusika na jinai za kivita katika vita ulivyoanzisha utawala huo ghasibu huko Ghaza tangu Oktoba 7, 2023 ambavyo hadi sasa vimeua karibu Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao kuna uwezekano wakakabiliwa na agizo la kukamatwa ni pamoja na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Vita Yoav Gallant, na Mkuu wa majeshi Herzi Halevi.../

 
 

 

Tags