May 08, 2024 11:43 UTC
  • Baadhi ya manusura watolewa chini ya vifusi baada ya jengo kuporomoka Afrika Kusini

Wafanyakazi wa huduma za uokoaji nchini Afrika Kusini leo walikuwa na matumaini ya kuwapata watu wengine wakiwa hai baada ya ripoti y awali kueleza kuwa waliwasiliana na angalau wafanyakazi 11 waliokwama kwenye vifusi baada ya jengo kuporomoka nchini humo Jumatatu wiki hii.

Watu wasiopungua saba wamethibitishwa kupoteza maisha katika ajali hiyo ya kuporomoka jengo la ghorofa tano katika eneo la George mashariki mwa mji wa Cape Town.

Mamlaka husika nchini Afrika Kusini zimeeleza kuwa wafanyakazi 26 hadi sasa wameondolewa katika eneo la ujenzi ulipokuwa ukifanyika ambako jengo la ghorofa tano liliporomoka Jumatatu wiki hii katika eneo la George umbali wa kilomita 400 mashariki mwa mji wa Cape Town huko katika pwani ya Afrika Kusini.  

Watu wengine 42 wanaaminika kuwa wamefunikwa chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka. Wafanyakazi wa huduma za uokoaji walikuwa na matumaini ya kuwafikia manusura wengi baada ya kusema kuwa mara kwa mara wamekuwa wakiwasiliana na wafanyakazi 11 waliosalia chini ya vifusi vya ghorofa tano lililoporomoka huko Cape Town.

Colin Deiner, mkuu wa huduma za usimamizi wa maafa katika jimbo la Western Cape, amesema kuwa operesheni ya utafutaji na uokoaji huenda ikachukua angalau siku tatu ili kuona kuwa watafanikiwa kuwatoa nje manusura ambao bado wako hai. 

Huduma za uokoaji zikiendelea 

Mamlaka husika nchini Afrika Kusini zimeanza uchunguzi ili kubaini kilichosababisha mkasa huo ambapo tayari polisi imefungua kesi ya jinai. Hata hivyo hakukuwa na taarifa za haraka kuhusu chanzo cha ajali hiyo ya kuporomoka jengo hilo.  Picha za CCTV kutoka kwenye nyumba iliyo karibu zilionyesha mfumo wa zege na kiunzi cha chuma kikiporomoka ghafla, na kusababisha vumbi zito lililoenea katika eneo la tukio. 

Tags