May 08, 2024 02:22 UTC
  • Hija ya kujibari na mushrikina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kwa kuzingatia Aya za Qur'ani Tukufu na kumbukumbu ya jina lililobarikiwa la Nabii Ibrahim (AS), ibada ya Hija ya mwaka huu inapaswa kuwa zaidi ya Hija ya kila mwaka, na inabidi iwe Hija na kutangazwa kujitenga au kujibari na adui wa Waislamu, Mzayuni mtenda uhalifu na wafuasi wake wa nchi za Marekani, Uingereza na Wamagharibi kwa ujumla.

Hija ni mojawapo ya ibada muhimu zaidi za kidini na kisiasa za Waislamu duniani kote ambapo amali ya kujibari na mushrikina ni kipengele muhimu zaidi cha kisiasa kwenye Hija.

Kiongozi Muadhamu akizungumza na wasimamizi wa Hija

Kujibari na mshirikina kunatokana na sisitizo la Qur’ani Tufuku la kuwa na uadui na maadui wa Mwenyezi Mungu na kufanya urafiki na marafiki wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alisema mwaka 2019 kwa mnasaba wa ibada ya Hija kwamba amali ya baraa au kujibari na mushrikina ambayo ina maana ya kuchukia ukatili, dhulma, maovu, ufisadi na dhulma ya mataghuti wa zama zote, ni moja ya baraka kubwa za Hija na fursa kwa mataifa ya Kiislamu yanayokandamizwa na maadui wa Uislamu. Lakini je, kwa nini  Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akaitaja Hija ya mwaka huu kuwa ni Hija kujibari?

Sababu kuu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kusisitiza kuwa baraa ya Hija ya mwaka huu ni maalumu na ya kipekee ni kutokana na jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza wanaoshambuliwa na kuuawa kinyama kila siku kwa uungaji mkono wa Marekani. Akizungumza mjini Tehran siku ya Jumatatu asubuhi mbele ya wasimamizi wa mahujaji wa Kiirani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa matukio haya yanayotokea Ukanda wa Gaza ni matukio ya kutisha na makubwa. Amesema kufichuliwa nyuso halisi za kundi la wamwagaji damu ambao wanatokana na tamaduni za Magharibi ni jambo ambalo halihusiani tu na zama na siku hizi bali litaendelea kubakia katika historia.

Utawala ghasibu wa Israel unaendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya siku 214 sasa. Kutokana na jinai hiyo, takriban watu elfu 35,000 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 78,000 wamejeruhiwa, ambapo asilimia 70 ya wahanga ni watoto na wanawake.

Vile vile miundombinu ya Ukanda wa Gaza imeharibiwa kabisa na utawala huo haramu ambapo kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, ukarabati wa ukanda huo utachukua miongo kadhaa kukamilika.

Watoto  wa Ukanda wa Gaza wanakufa kwa njaa na maradhi, na utawala wa Kizayuni hauruhusu kutumwa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.  Mhusika mwingine mkuu  wa jinai hizo dhidi ya watu wa Gaza ni serikali ya Marekani na Wamagharibi.
Serikali ya Marekani mbali na kuwa inauunga mkono waziwazi utawala wa Kizayuni kwa upande wa kijeshi na kiuchumi, pia inatumia vibaya nafasi yake katika mfumo wa dunia kwa kuzuia hatua zozote za kimataifa zinazolenga kukomesha mauaji ya kimbari ya Wazayuni huko Gaza.

Jinai za Wazayuni Gaza

Akizungumza siku ya Jumatatu mbele ya wasimamizi wa Mahujaji wa Kiirani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alihoji kwamba, je, ni nani katika dunia ya leo anayewafanyia uadui Waislamu, anawashambulia na kuwaua? Ni nani anayewafukuza wanawake, wanaume na watoto wao kutoka makazi na ardhi zao? Ni nani huyo? Je, adui wa Kizayuni aarifishwe kuliko hivi katika Qur'ani Tukufu? Si adui Mzayuni pekee, bali pia na wale wote wanaomsaidia. Je, ni nani hao wanaomsaidia?

Lau isingekuwa msaada wa Marekani je, utawala wa Kizayuni ungekuwa na uwezo na ujasiri wa kuwaua kinyama namna hii Waislamu, wanaume, wanawake na watoto katika eneo finyu kabisa kama hilo? Hatuwezi kuamiliana vizuri na adui huyu.

Haiwezekani kuwa na huruma na watu hawa, iwe ni wale wanaohusika na mauaji moja kwa moja, au wale wanaowasaidia wauaji. Wale wanaoharibu nyumba au wanaowasaidia wanaoharibu nyumba hizo.

Ni kwa kuzingatia hali hiyo, ndipo baraa katika Hija ya mwaka huu ikapewa umuhimu mkubwa zaidi na wa kipee na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduiz ya Kiislamu.