May 07, 2024 08:17 UTC
  • Safari ya Grossi nchini Iran na kuwekwa wazi maendeleo ya amani ya nishati ya nyuklia ya Iran

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA aliwasili mjini Tehran Jumatatu akiongoza ujumbe alioandamana nao kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa nyuklia na vilevile kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nyuklia na kisiasa wa nchini.

Grossi pia atakutana na kufanya mazungumzo na Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya kiislamu ya Iran. Katika safari yake ya siku mbili nchini, Grossi pia Jumatatu alasiri alielekea mjini Isfahan ambapo pamoja na mambo mengine alishiriki katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa nyuklia, akazungumza na Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na kujibu maswali ya waandishi wa habari.

Safari ya Grossi inafanyika katika hali ambayo eneo la Asia Magharibi linashuhudia mgogoro mkubwa wa kiusalama na kisiasa kutokana na  utawala wa Kizayuni kuendeleza vita vya umwagaji damu huko Gaza, na wakati huo huo kushuhudia kwa mara ya kwanza makabiliano ya moja kwa moja kati ya Iran na utawala wa Kizayuni kupitia operesheni ya Ahadi ya Kweli, iliyotekelezwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kujibu mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.

Rafael Grossi

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umekuwa ukisisitiza mara kwa mara katika ripoti zake kuwa mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ni wa amani na kuwa hautekelezwi kwa malengo ya kijeshi. Pamoja na hayo lakini Tel Aviv, pamoja na Washington, bado zinaendelea kuituhumu Tehran kuwa inajaribu kujipatia silaha za nyuklia. Kwa hakika, mbali na tuhuma zisizo na msingi za Wamagharibi kuhusiana na jaribio la Tehran la kujipatia silaha za nyuklia, Iran imeweza kunufaika pakubwa na kwa malengo ya amani na teknolojia ya nyuklia katika nyanja mbalimbali zikiwemo za uzalishaji umeme, dawa, kilimo na nyanja nyinginezo.

Kile kinachosababisha wasiwasi wa Marekani na washirika wake kuhusu suala la nyuklia ni hatua zilizochukuliwa na Iran baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya JCPOA. Ingawa, Iran ilijitolea kutekeleza kikamilifu ahadi zake na kupunguza shughuli zake za nyuklia kwa miaka kadhaa kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, lakini katika kipindi cha urais wa Donald Trump mnamo Mei 2018, Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano hayo na kuiwekwa Iran vikwazo vikali zaidi, ikiwa ni katika fremu ya kutoa mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran. Kwa kuzingatia uamuzi wa wanachama wa Ulaya wa kundi la 4+1 kutoheshimu ahadi zao kuhusu mapatano hayo, Tehran kwanza ilipunguza ahadi zake za nyuklia katika hatua 5 na kisha, kuchukua hatua mpya za kujiimarisha katika uwanja wa nyuklia kwa mujibu wa sheria ya Majlis ya Ushauri ya Kiislamu. Miongoni mwa mambo yanayoweza kutajwa katika muktadha huo ni urutubishaji wa asilimia 20 na kisha asilimia 60 wa madini ya urani na kustawishwa taasisi za nyuklia, jambo ambalo lilizitia wasiwasi mkubwa Washington na washirika wake wa kieneo hususan utawala wa Kizayuni. Kupunguzwa  kiwango cha ushirikiano na wakala wa IAEA katika muktadha wa kusimamishwa utekelezaji wa itifaki ya ziada pia kulifanyika katika fremu ya utekelezaji wa sheria ya Bunge la Iran ikiwa ni katika kukabiliana na siasa za nchi za Ulaya za kutotekeleza ahadi zao kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo katika mazungumzo ya  Vienna yaliyofanyika kwa ajili ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran, Tehran ilitangaza na bado inatilia mkazo kuwa iko tayari kutekeleza kikamilifu majukumu yake chini ya mpango wa JCPOA iwapo masharti yake ikiwa ni pamoja na kuondolewa vikwazo na kurejea Marekani katika  JCPOA yatazingatiwa na kupewa kipaumbele.

Image Caption

 

Wakati huo huo, Tehran, kwa kuanda mkutano wa 30 wa Kitaifa wa Nyuklia na kikao cha kwanza cha Kimataifa cha Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia 2024 kuanzia Mei 6 hadi 8 huko Isfahan, sambamba na kuonyesha maendeleo ya nyuklia ya Iran, imeandaa uwanja wa wataalamu kutoka nchi mbalimbali za dunia kubadilishana mitazamo na fikra katika uwanja huo. Akigusia kuhudhuria watafiti 50 wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali katika kikao hicho, Javad Karimi Sabet, Mkuu wa Jumuiya ya Nyuklia ya Iran amesema: Kiwango cha ushiriki wa mashirika ya ndani na nje katika kikao hicho kilikuwa cha juu kuliko ilivyotarajiwa. Karimi Sabet amesema: Kushiriki Rafael Grossi katika kikao cha Kwanza cha Kimataifa cha Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia ya Iran huko Isfahan ni uthibitisho wa uungaji mkono wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa vikao vya kisayansi vya Iran.

Kwa hakika, safari ya Grossi nchini Iran na kushiriki kwake katika kongamano hilo la kimataifa la Isfahan, safari ambayo imefanyika katika mazingira ambayo utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Wamagharibi unaeneza propaganda kali za kisiasa na kisaikolojia dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, mbali na kuwa ni muhuri wa wakala huo kuthibitisha kuwa shughuli za nyuklia za Iran ni salama, pia inaonyesha maendeleo makubwa ambayo Iran imeweza kuyafikia katika uwanja wa teknolojia ya nishati ya nyuklia, ambayo, kwa kweli yanatokana kikamilifu na vipaji vya wataalamu wa humu humu nchini bila kutegemea nchi za kigeni.

Tags