May 07, 2024 06:36 UTC
  • Bunge la Misri: Israel haina haki ya kuchukua hatua za kijeshi katika mji wa Rafah

Sambamba na vitisho vilivyotolewa na utawala haramu wa Kizayuni vya mashambulizi ya ardhini dhidi ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Bunge la Misri limetangaza kwamba mapatano ya Camp David hayaruhusu Israel kuchukua hatua za kijeshi huko Rafah.

Kwa mujibu wa gazeti la Misri la Al-Ahram, Meja Jenerali Ahmad Al-Awadi, Mkuu wa Kamisheni ya Ulinzi na Usalama wa Taifa katika Bunge la Misri, amesema, usalama wa taifa ni mstari mwekundu kwa Misri mbali na kwamba suala la Palestina lina nafasi ya kwanza katika vipaumbele vya nchi hiyo.

 

Al-Awadi ameongeza kuwa, makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya Cairo na Tel Aviv (Camp David) hayairuhusu Israel kuchukua hatua yoyote katika eneo la mpakani kati ya Ukanda wa Gaza na Misri hasa katika mhimili wa Salah al-Din (Philadelphia), isipokuwa tu kama Misri itaafiki jambo hilo. Isitoshe, kulingana na vipengee mkataba huo wa amani Cairo haitaruhusu katika hali yoyote ile jeshi la  Israel kuingia katika maeneo ambayo hayajaruhusiwa.

Mkuu wa Kamisheni ya Ulinzi na Usalama wa Taifa katika Bunge la Misri ametahadharisha kuhusu hatua zozote watakazo chukua wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni katika mji wa Rafah ambazo zitasababisha mauaji katika mji huo na kuulemaza Ukanda wa Gaza, na akataka utekelezwe usitishaji wa vita na kudumisha amani ili kuepusha mapigano mapya katika eneo.