Mar 21, 2024 10:12 UTC
  • UN: Sudan kukumbwa na mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuwa, mapigano makali ya karibu mwaka mmoja sasa kati ya makundi mawili hasimu, yaani Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yameiweka nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika ncha ya kutumbukia kwenye mgogoro mbaya zaidi wa njaa duniani.

Edem Wosornu, Mkurugenzi wa operesheni za kibinadamu wa OCHA ameliambia Baraza la Usalama la UN kuwa, thuluthi moja ya jamii yote ya Wasudan (watu milioni 18), wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula kwa kiwango cha kuogofya.

Amesema, "Tathmini ya karibuni inaonesha kuwa, mtoto mmoja anafariki dunia ndani ya kila saa mbili, katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam mjini El Fasher, eneo la Darfur Kaskazini."

Wosornu amesema washirika wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu wanakisia kuwa watoto karibu 222,000 huenda watapoteza maisha kutokana na utapiamlo katika wiki na miezi michache ijayo nchini Sudan.

Kwa mujibu wa OCHA, mamilioni ya Wasudan wamevuka mpaka na kuingia Sudan Kusini na katika nchi nyingine jirani tangu mapigano yalipoanza Aprili 15 mwaka jana 2023 huko Sudan.

Mgogoro wa wakimbizi nchini Sudan

Naye Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, mbali na watu milioni 18 kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula ndani ya Sudan, lakini watu wengine milioni 7 wanasumbuliwa na njaa katika nchi jirani ya Sudan Kusini na wengine milioni 3 nchini Chad, katika mpaka wa Darfur. 

Takwimu za UN zinaonesha kuwa, mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na Kamanda Hamdan Dagalo yameshaua watu karibu 14,000 hadi sasa, na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan huku watu milioni 25 wakihitaji misaada ya dharura.

 

Tags