Hali mbaya ya wakimbizi wa Afghanistan nchini Marekani na Ulaya
Kufuatia matukio ya kisiasa huko Afghanistan na Taliban kudhibiti hali ya mambo nchini humo, maelfu ya raia wa nchi hiyo waliamua kukimbilia Marekani na nchi za Ulaya wakidhani kuwa wangepata usalama na maisha mazuri huko.
Lakini kinyume na walivyodhani, wangi wao wamewekwa na kulazimika kuishi katika maeneo ya mipakani na katika kambi za wakimbizi zisizokuwa na suhula za kutosha za afya na za kuendeshea maisha. Hali hiyo imepelekea idadi kubwa ya Waafghani waliokimbilia Uingereza kukosoa siasa za nchi hiyo kuhusu wakimbizi na kutaka wareheshwe nchini kwao.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, Waafghani wengi waliojumuishwa katika operesheni ya kuwahamisha raia wa Uingereza kutoka Afghanistan, sasa wanasema wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kwenye hoteli wanakozuiliwa kiasi kwamba hawawezi tena kuvumilia hali hiyo. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita serikali ya London ilitangaza mpango wa eti 'kuwapa mapokezi mazuri' wakimbizi wa Kiafghani lakini hadi sasa hayo yamebakiwa kuwa ni maneno matupu tu yasiyotekelezwa kivitendo.
Wakimbizi wa Kiafghani waliokimbilia katika nchi nyingine za Ulaya pia wanakabiliwa na hali kama hiyo. Katika hali ambayo Josep Borrell, mkuu wa siasa za kigeni wa Umoja wa Ulaya amezitaka nchi za umoja huo zipokee wakimbizi wa Kiafghani kati ya elfu kumi hadi ishirini, lakini taasisi za umoja huo tayari zimezitaka nchi 12 wanachama zigharamie mpango wa kujenga ukuta na uzio utakaozuia wakimbizi kuingia katika mipaka ya nchi wanachama.
Nchi nyingi za Ulaya Mashariki wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zinatekeleza mipango ya kujenga ukuta wenye urefu wa malefu ya kilomita katika mipaka yao kwa gharama ya umoja huo. Kama ilivyofanya Ugiriki, nchi hizo zimeazimia kujenga kuta na vizuizi katika mipaka yao ili kuwazuia wakimbi kuingia katika nchi hizo.
Viongozi wa Ugiriki tayari wamefungua kambi ya wakimbi ya kwanza kati ya kambi tano kama hizo zinazotazamiwa kufunguliwa karibuni kwa ajili ya kurundikwa humo wakimbizi wa kigeni, jambo ambalo limekosolewa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu. Kambi hiyo ambayo inapatikana katika kisiwa cha Samos imezungukwa na nyaya za miba na mifumo ya kiusalama ya kielektroniki. Kuhusu hilo, mmoja wa maafisa wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amekosoa mbinu zinatumika kuendesha kambi hiyo na kusema wakimbizi ni watu wanaopasa kulindwa na kusaidiwa na wala hawahatarishi jamii kama wanavyofanya wahalifu.
Ylva Johansson, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Umoja wa Ulaya, amesema ameona nchi nyingi zikianzisha vizuizi hivyo na kwamba anadiriki na kuafikiana nazo katika jambo hilo. Hii ni katika hali ambayo Filippo Grande, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi amesema kwa mujibu wa tathmini zilizopo, Waafghani elfu 85 wanatazamiwa kukimbia nchi yao katika miaka mitano ijayo na kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kuwapa hifadhi na makazi nusu ya wakimbizi hao. Tangu mwaka 2015 hadi sasa Waafghani wapatao elfu 570 wameomba hifadhi katika nchi 27 wanachama wa umoja huo.
Waafghani wengi waliokimbilia Marekani pia wanaishi katika hali mbaya na ya kusikitisha. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na jeshi la Marekani, Waafghani wapatao elfu 53 waliohamishiwa nchini humo baada ya Taliban kuteka mji mkuu wa nchi yao, Kabul, sasa wanaishi katika mazingira magumu katika kambi nane za jeshi hilo.
Wakimbizi waliohamia Marekani wanaishi katika hali mbaya na ya kisikitisha lakini pamoja na hayo wanakabiliwa na hatari ya kushambuliwa na magenge ya wabaguzi wa rangi nchini humo. Karibuni wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani iliwatahadharisha polisi kwamba huenda uwepo wa wakimbizi wa Kiafghani nchini humo ukazua mzozo wa kijamii na kuyachochea makundi ya wabuguzi wa rangi kutumia mabavu dhidi yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, magenge ya wabaguzi wa rangi yameonekana yakiendesha harakati za kutiliwa shaka kiusalama karibu na vituo na idara za serikali kuu ya Marekani zinazotoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Magenge hayo yamekuwa yakitoa taarifa za kutaka kuchomwa moto taasisi zisizo za serikali katika jimbo la Florida ambazo zimekuwa na mchango katika kuwasaidia wakimbizi wa Afghanistan.
Maelfu ya wakimbizi wengine wa Kiafghani pia wanaishi katika mazingira mabaya katika kambi za wakimbi huko Ujerumani, Qatar, Imarati, Albania na Uganda bila kujua mustkbali unaowasubiri.