Guterres: Afghanistan imekumbwa na mgogoro usioelezeka wa kibinadamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuwaokoa wananchi wa Afghanistan na kusisitiza kuwa, nchi hiyo hivi sasa imo kwenye mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao hauelezeki hivyo hatua za haraka lazima zichukuliwe kuepusha kutokea janga kubwa la kibinadamu nchini humo.
António Guterres alisema hayo jana katika mkutano uliofanyika hapa mjini Tehran kwa njia ya Intaneti baina ya majirani wa Afghanistan na sambamba na kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuitisha mkutano huo amesema kuwa, wananchi wa Afghanistan wanastahiki kuwa na serikali itakayoshirikisha pande zote, itakayochunga haki za binadamu na kuzingatia vilio na maslahi ya wananchi.
Siku chache zilizopita pia mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yalitangaza kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula. Taarifa ya mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa, zaidi ya wananchi milioni 22 wa Afghanistan watakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula katika msimu wa baridi mwaka huu.
Nalo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa, katika msimu huu wa baridi kali, mamilioni ya Waafghani watalazimika kuchagua baina ya kuhajiri au kufa kwa njaa. Omar Abdi Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) alisema hivi karibuni kuwa, mfumo wa afya na huduma za kijamii nchini Afghanistan unakaribia kusambaratika.
Itakumbukwa kuwa, mkutano wa pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan+Russia umefanyika hapa mjini Tehran kwa shabaha ya kujadili changamoto mbambali zinazoikabili nchi hiyo baada ya majeshi ya Marekani kuondoka nchini humo na wanamgambo wa Taliban kuchukua hatamu za uongozi wa nchi.