Unicef kuwalipa mishahara walimu moja kwa moja nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76542-unicef_kuwalipa_mishahara_walimu_moja_kwa_moja_nchini_afghanistan
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umesema kuwa unafanya mpango wa kuanzisha mfumo ambao utawafadhili kifedha moja kwa moja walimu nchini Afghanistan. Hiyo ni baada ya jamii ya kimataifa kuzuia fedha kwa utawala wa kundi la Taliban linaloongoza nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 04, 2021 23:54 UTC
  • Unicef kuwalipa mishahara  walimu moja kwa moja nchini Afghanistan

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umesema kuwa unafanya mpango wa kuanzisha mfumo ambao utawafadhili kifedha moja kwa moja walimu nchini Afghanistan. Hiyo ni baada ya jamii ya kimataifa kuzuia fedha kwa utawala wa kundi la Taliban linaloongoza nchi hiyo.

Jeannette Vogelaar Mkurugenzi wa Elimu wa Unicef nchini Afghanistan ameeleza kuwa, shirika hilo linaandaa mpango ambao utaruhusu malipo ya moja kwa moja kuwafikia walimu bila ya mishahara yao kupitia kwa mamlaka iliyoko madarakani.  

Katika mkakati wake wa awali shirika la Unicef limesema kuwa litaanza kuwasajili walimu wote wa shule za serikali. Bi Jeannette ameongeza kuwa, njia bora ya kusaidia elimu kwa watoto wa kike nchini Afghanistan ni kuendelea kuzisadia shule na walimu wao. "Unicef inawatolea wito wafadhili kutowaangusha watoto wa Kiafghani," amesema Mkurugenzi wa Elimu wa shirika la Unicef huko Afghanistan. 

Huduma za umma nchini Afghanistan hususan sekta za afya na elimu zimetumbukia katika mgogoro tangu kundi la wanamgambo wa Taliban lichukue madaraka ya nchi hiyo Agosti 15 mwaka huu. Nchi nyingi za kigeni zimekata misaada ya kifedha kwa Afghanistan isipokuwa misaada ya kibinadamu. 

Wakati huo huo mabilioni ya dola za Benki Kuu ya Afghanistan ambazo zilihamishiwa nje ya nchi pia zimezuiwa. Inafaa kuashiria hapa kuwa, shule za upili za wasichana katika maeneo mengi nchini Afghanistan zimefungwa huku zile za wavulana zikiendelea na masomo. 

Wavulana wakiwa darasani nchini Afghanistan