Mauaji na uhalifu wa kutumia mabavu vyaongezeka nchini Marekani
Vitendo vya mauaji na uhalifu wa kutumia mabavu vinaripotiwa kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya Marekani na kuwafanya wananchi wa hiyo kuendelea kukabiliwa na moja ya matatizo makubwa ya kijamii katika nchi hiyo.
Kanali ya Televisheni ya Fox News imetangaza kuwa, maafisa wa serikali wamekuwa wakikabiliwa na kuongezeka vitendo vya mauaji na uhalifu wa kutumia mabavu katika akthari ya miji ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya kanali hjiyo ya televisheni ni kuwa, uhalifu wa aina tofauti umeendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini Marekani huku serikali za kieneo zikijaribu kupambana na hali hiyo bila mafanikio.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, vitendo vya mauaji na uhalifu wa kutumia mabavu vimeongezeka pakubwea ikilinganishwa na mwaka uliopita (2020).
Mwezi Mei mwaka huu, Polisi ya Federali ya Marekani FBI ilitangaza habari ya kuongezeka kwa asilimia 25 vitendo vya uhalifu na jinai nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti za FBI zilizotangazwa na televisheni ya CNN huko Marekani, katika kipindi cha miezi mitatu ya awali ya mwaka huu wa 2021 idadi ya vitendo vya uhalifu nchini humo viliongezeka kwa asilimia 18 mwezi Mei mwaka huu ikilinganishwa na muda kama huo mwaka uliopita.
Maelfu ya watu wanauawa na kujeruhiwa kwa risasi kila mwaka katika maeneo tofauti ya Marekani. Ripoti rasmi za serikali za nchi hiyo zinaonesha kuwa silaha zinazomilikiwa na raia nchini Marekani ni baina ya milioni 270 hadi milioni 300, yaani kila raia wa Marekani kwa uchache anamiliki silaha moja ya moto.