Jan 16, 2022 07:59 UTC
  • Maelfu waandamana Ulaya kupinga chanjo ya lazima ya Covid-19

Maelfu ya wananchi wa Austria wamejitokeza mabarabarani katika maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya kuwalazimisha wananchi kupiga chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Waandamanaji hao wamesema wanapinga vikali hatua ya serikali ya kuwataka wananci waoneshe vyeti vya kuthibitisha kuwa wamechanja katika usafiri wa umma, na vile vile kabla ya kuingia katika maeneo ya umma na binafsi.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yanayoitaka serikali ya nchi hiyo ijiuzulu, wakisisitiza kuwa chanjo hiyo inapaswa kuwa ya khiari.

Bunge la Austria wiki ijayo linatazamiwa kupiga kura ya kupasisha sheria ya kuweka chanjo dhidi ya corona kuwa ya lazima, na iwapo sheria hiyo itapasishwa, nchi hiyo itakuwa ya kwanza barani Ulaya kuchukua hatua hiyo.

Ingawaje serikali ya Austria haijasema itawapiga kwa nguvu chanjo wananchi wake, lakini wale wanaokataa kupigwa chanjo hiyo wanatuhumiwa kuhujumu mfumo wa afya wa nchi hiyo, na watapigwa faini ya Euro 600, na kiasi hicho kinaweza kuongezeka hadi Euro 3,600.

Maandamano ya Paris

Wakati huohuo, maandamano makubwa yalishuhudiwa jana Jumamosi pia Paris, mji mkuu wa Ufaransa, kupinga azma ya serikali ya kuongeza mbinyo na vikwazo dhidi ya watu ambao hawajachanja nchini humo.

Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika nchi za Italia na Uswisi, kupinga hatua ya serikali za nchi hizo za Ulaya ya kuwataka watu wote wawe na pasi ya kuthibitisha kuwa wamepokea chanjo ya Corona, ili waruhusiwe kazini  na katika maeneo ya umma.

Tags