Chuo kingine India chazuia wanafunzi Waislamu kuvaa Hijabu
Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kuendekeza misimamo ya chuki na kufurutu ada ya serikali ya waziri mkuu wa India Narendra Modi, wanafunzi Waislamu wanaovaa hijabu wamepigwa marufuku kuingia madarasani katika chuo kimoja katika jimbo la Karnataka, kusini mwa India.
Video iliyosambaa mitandaoni inaonesha mwalimu mkuu akiwazuia makumi ya wanafunzi wa kike Waislamu waliovaa vazi la staha la hijabu kuingia madarasani. Wanafunzi hao wamesema wamezuiwa kuingia madarasani katika kipindi nyeti cha mitihani, jambo ambalo linatishia mustakabali wao.
Chuo hicho kimewapiga marufuku wanafunzi Waislamu kuingia madarasani wakiwa wamevaa hijabu kwa kisingizio kwamba vazi hilo pamoja na kitambaa cha nikabu havimo kwenye orodha ya mavazi rasmi yanayokubalika kuvaliwa chuoni hapo.
Shashi Tharoor, mbunge wa chama cha upinzani cha Congress amejiwa juu ya wafuasi wa chama tawala cha Bharatiya Janata, kwa kutaka maelezo ya kwa nini wanafunzi wengi wanaruhusiwa darasani wakiwa wamevaa nembo za kidini kama msalaba na alama nyekundu kwenye paji la uso kwa wanachuo Wahindu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, wanachuo Waislamu wanaovaa hijabu walipigwa marufuku kuingia madarasani katika chuo cha serikali cha Udupi kilichoko kwenye jimbo la Karnataka kusini-magharibi ya India.
Tukio la wanafunzi Waislamu kupigwa marufuku kuvaa hijabu madarasani si la kwanza kuripotiwa katika miaka ya karibuni kwenye jimbo la Karnataka. Mbali na Udupi, matukio sawa na hayo yameripotiwa pia katika vyuo vya miji ya Dakshina, Kannada na Chikkamagaluru.