WFP: Mamilioni wanakabiliwa na njaa Pembe ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80128-wfp_mamilioni_wanakabiliwa_na_njaa_pembe_ya_afrika
Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 13 katika eneo la Pembe ya Afrika wanakabiliwa na njaa kali. Hayo yameelezwa leo Jumanne na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2022 09:21 UTC
  • WFP: Mamilioni wanakabiliwa na njaa Pembe ya Afrika

Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 13 katika eneo la Pembe ya Afrika wanakabiliwa na njaa kali. Hayo yameelezwa leo Jumanne na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP).

Hali ya ukame imeziathiri jamii za wafugaji na wakulima katika maeneo ya kusini na kusini mashariki mwa Ethiopia, kusini mashariki na kaskazini mwa Kenya na kusini kati mwa Somalia; huku uhaba wa mvua za chini ya kiwango cha wastani ukitishia kuzidisha hali mbaya katika miezi ijayo. 

Michael Dunford Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki ameeleza kuwa, mavuno yameharibikwa, mifugo imekufa na ukosefu wa chakula unazidi kuongezeka kutokana na ukame mtawalia uliozikumba nchi za eneo la Pembe ya Afrika. 

Nchi za Pembe ya Afrika zilizoathiriwa na ukame

Dunford amesema kuwa, "hali hii inahitajia hatua za haraka na msaada madhubuti ili kuimarisha jamii kwa ajili ya siku za usoni." Uhaba wa maji na kukosekana malisho ya mifugo vilivyosababishwa na uhaba wa mvua kama ilivyotarajiwa vimepunguza mavuno ya mazao na kupelekea kufariki mifugo mingi. 

Wakati huohuo kupanda kwa bei za vyakula, mdodoro wa kiuchumi n.k kumepunguza uwezo wa watu wa kununua chakula. WFP inasema kuwa, familia sasa zinalazimika kuhama makazi yao; suala linalopelekea kuongeka migogoro baina  ya jamii. Si hayo tu bali tatizo la utapiamlo pia bado ni la kiwango cha juu katika Pembe ya Afrika na huwenda likaongezeka iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. 

Mapema mwezi huu, Shirika la Unicef liliripoti kuwa, watu zaidi ya milioni sita huko Ethiopia watahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu hadi kufikia katikati ya mwezi Machi mwaka huu.