White House: Mazungumzo ya Vienna yamefikia kwenye hatua nyeti na hasasi
Msemaji wa Ikulu ya rais wa Marekani, White House, sambamba na kuanza tena duru mpya ya mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 4+1 amesema, mazungumzo hayo yamefikia hatua nyeti na hasasi.
Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na vya kinyume cha sheria ilivyowekewa Iran, ilianza tena Jumanne ya tarehe 8 Februari baada ya kusitishwa kwa kipindi kifupi ili kutoa fursa kwa pande husika kwenda kufanya mashauariano kwenye miji yao mikuu ya kuchukua maamuzi ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari na pasi na kuashiria chochote kuhusu majukumu yanayopasa kutekelezwa na Marekani ili iweze kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kufidia hasara ilizosababisha kwa kuhalifu majukumu yake, msemaji wa White House Jen Psaki amesema, mazungumzo na Iran kuhusiana na kurudi pande zote mbili kwenye utekelezaji wa majukumu ya JCPOA yamefikia hatua hasasi.
Katika kufanikisha mbinu ya Washington ya sera za utoaji muhula bandia wa mwisho wa mazungumzo ili kuishinikiza timu ya wawakilishi wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia, Psaki amedai kuwa ikiwa makubaliano hayataweza kufikiwa katika muda wa wiki kadhaa zijazo, kutokana na hatua za nyuklia inazoendelea kupiga Iran, haitawezekana kurudi tena kwenye makubaliano ya JCPOA.
Awali kabla ya hapo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, naye pia alidai kuwa dirisha la fursa ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna linaanza kujifunga.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ni nchi inayotekeleza majukumu na masuulia yake, imeshatangza mara kadhaa kuwa, kwa vile Marekani ndiyo iliyokiuka makubaliano ya JCPOA, ndiyo yenye wajibu wa kuondoa vikwazo ilivyoweka ili iweze kurejea kwenye makubaliano hayo; na kuna ulazima pia wa kuwepo utaratibu wa kuthibitisha kama kweli Washington imetekeleza ahadi zake.../