Maandamano ya kulaani marufuku ya hijabu shuleni yaenea kote India
Maandamano ya kulaani hatua ya skuli kadhaa katika jimbo la Karnataka kusini mwa India kuwazuia wasichana Waislamu wanaovaa hijabu wasiingie madarasani kwa kisingizio cha kutekeleza amri ya wizara ya elimu ya jimbo hilo, yameenea katika pembe mbalimbali za nchi hiyo ya Asia.
Maandamano hayo yameshuhudiwa katika kona mbalimbali za nchi hiyo, huku waandamanaji wakibeba mabango yenye jumbe za kulaani marufuku ya uvaaji hijabu iliyowekwa katika taasisi za elimu za jimbo la Karnataka.
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanawake Waislamu katika barabara za Jaipur jimboni Rajasthan wakati wa maandamano hayo yalikuwa yameandikwa: Hijabu ni utambulisho wangu na elimu ni haki yangu; na Hijabu yangu haifanyi nisiwe raia kamili wa India.
Marufuku ya kuvaa hijabu iliyowekwa katika vyuo vya jimbo la Karnataka imeamsha wimbi la hasira za wanafunzi Waislamu, ambao wanasema, hiyo ni hujuma inayolenga imani yao ambayo inatambuliwa rasmi na katiba ya India.

Hii ni katika hali ambayo, makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia yanatumia mabavu kuwazuia mabanati wa Kiislamu wasiingie vyuoni na hivyo kuibua mivutano ya kijamii jimboni humo.
Serikali ya jimbo la Karnataka inayoongozwa na chama cha mrengo wa kulia cha Bharatiya Janata (BJP) hivi karibuni ilitangaza kufunga taasisi za elimu kwa muda wa siku tatu kutokana na kushtadi mzozo huo.