Russia yamfukuza Naibu Balozi wa Marekani mjini Moscow
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80474-russia_yamfukuza_naibu_balozi_wa_marekani_mjini_moscow
Russia imemtimua mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani nchini humo, wakati huu ambapo nchi mbili hizo zinaendelea kuzozana kuhusu madai ya Wamagharibi kuwa serikali ya Moscow ina azma ya kuivamia kijeshi Ukraine.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 17, 2022 23:37 UTC
  • Russia yamfukuza Naibu Balozi wa Marekani mjini Moscow

Russia imemtimua mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani nchini humo, wakati huu ambapo nchi mbili hizo zinaendelea kuzozana kuhusu madai ya Wamagharibi kuwa serikali ya Moscow ina azma ya kuivamia kijeshi Ukraine.

Shirika rasmi la habari la Russia la TASS limeripoti hayo na kueleza kuwa, Moscow imemfukuza Bart Gorman, Naibu Balozi wa Marekani nchini Russia.

Hata hivyo ripoti hiyo haijatoa maelezo zaidi kuhusu uamuzi huo wa Russia wa kumtimua mwanadiplomasia huyo wa Marekani. Ubalozi wa Marekani nchini Russia umesema Washington inajiandaa kujibu mapigo kwa hatua hiyo ya Moscow.

Mgogoro katika uhusiano wa Russia na nchi za Magharibi hasa Marekani umekuwa mkubwa sana katika wiki za hivi karibuni hasa baada ya baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya na Marekani kudai kuwa Russia ina nia ya kuivamia kijeshi Ukraine. 

Vikosi vya Russia karibu na mpaka wa Ukraine

Hii ni katika hali ambayo, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza mara kadhaa kuwa nchi yake haitaki kutokee vita barani Ulaya wala nchini Ukraine na ni kwa sababu hiyo ndio maana imetoa pendekezo la kudhaminiwa usalama wa eneo hilo.

Moscow inasisitiza kuwa, lengo la Marekani na nchi za Magharibi la kueneza propaganda hizo ni kuzusha hali ya wasiwasi tu katika eneo hilo.