Maelfu ya Wamarekani wajisajili kwenda kupigana Ukraine
Maelfu ya wananchi wa Marekani wameuandikia barua ubalozi wa Ukraine mjini Washington wakiomba kuruhusiwa kwenda kupigana na jeshi la Russia wakishirikiana na wanajeshi wa Ukraine.
Afisa wa kijeshi katika ubalozi huo ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, mpaka sasa ubalozi huo umepokea maombi kutoka kwa Wamarekani 3,000 wanaotaka kwenda kushiriki vita vinavyoendelea Ukraine.
Habari zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa waliotuma barua hizo ni maveterani wa kijeshi pamoja na raia wa kawaida, wanaodai kuwa wako tayari kwenda Ukraine kushiriki vita na eti shughuli za kibinadamu.
Wadadisi wa mambo wamekosoa undumakuwili wa Marekani na nchi za Magharibi, ambazo kwa upande mmoja zinachochea moto wa mgogoro wa Ukraine, na kwa upande mwingine zinaituhumu Russia kuwa ndiyo inayoshadidisha mgogoro huo.
Viongozi wa Marekani akiwemo Seneta wa chama cha Republican, Lindsey Graham wametoa mwito hadharani wa kuuawa kigaidi Rais Vladmir Putin wa Russia, wakidai kuwa hiyo tu ndiyo njia ya kusimamisha mzozo wa Ukraine.
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Ukraine inaendelea kutoa hifadhi kwa magaidi wa kimataifa, wakiwemo wale waliopigana nchini Syria. Siku chache zilizopita, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alizishukuru nchi waitifaki kwa kuendelea kutuma silaha na zana za vita nchini humo na kusema kundi la kwanza la wapiganaji elfu 16 wa kigeni limewasili nchini Ukraine.
Ripoti zinasema operesheni maalumu ya jeshi la Russia nchini Ukraine ambayo inafanyika kwa ajili ya kuipokonya silaha serikali ya nchi hiyo, inalenga pia kupambana na makundi ya kigaidi.