Umoja wa Ulaya waonesha matumaini ya kufikiwa makubaliano kuhusu JCPOA
(last modified Sat, 19 Mar 2022 02:48:52 GMT )
Mar 19, 2022 02:48 UTC
  • Umoja wa Ulaya waonesha matumaini ya kufikiwa makubaliano kuhusu JCPOA

Msemaji wa Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amesema kuwa, ana imani mazungumzo ya Vienna yatazaa matunda mazuri na yatapelekea kuondolewa vikwazo Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Peter Ustinov alisema hayo jana Ijumaa mbele ya waandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji na kuongeza kuwa, Umoja wa Ulaya bado una imani ya kufikiwa makubaliano mazuri katika mazungumzo ya Vienna na unaendeleza juhudi zake za kuhakikisha mazungumzo hayo yanafikia natija iliyokusudiwa.

Awamu wa nane ya mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Iran iliyoanza tarehe 8 mwezi uliopita wa Februari  iliingia kwenye mapumziko mengine tena Ijumaa ya tarehe 11 mwezi huu wa Machi kwa ajili ya mashauriano zaidi.

Mazungumzo hayo yalipata msukumo na kupiga hatua nzuri kutokana na ubunifu wa Iran. Hata hivyo nchi za Magharibi zimekuwa zikikwamisha mara kwa mara juhudi za kumaliza haraka mazungumzo hayo. Itakumbukwa kuwa, Marekani ndiyo iliyojitoa - tena kijeuri - katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na baadaye kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo ya kimataifa ambayo Marekani ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha.

Mazungumzo ya Vienna kuhusu JCPOA

 

Peter Ustinov pia amesema, Umoja wa Ulaya unazungumza na kushirikiana na pande zote ili kuhakikisha vikwazo ilivyowekewa Iran, vinaondolewa.

Matamshi ya viongozi wa nchi za Magharibi kuhusiana na kukaribia mno kufikiwa makubaliano mjini Vienna, Austria kuhusu mapatano ya JCPOA yametolewa katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, amesema kuwa Tehran itaendelea kusimama imara kulinda mistari yake myekundu kwenye mazungumzo hayo.

Tags