Biden: Siombi radhi wala sibadili kauli yangu kuhusu Putin
Rais Joe Biden wa Marekani amesema, haombi radhi wala hatobadili kauli yake kuhusu aliyosema kwamba Rais Vladimir Putin wa Russia hapasi kubaki madarakani.
Siku ya Jumamosi, wakati akiwa nchini Poland mwishoni mwa safari yake ya siku nne barani Ulaya, Biden alivielezea vita vinavyoendelea hivi sasa nchini Ukraine kuwa ni sehemu ya mapigano kwa ajili ya uhuru na kisha akatamka kinagaubaga kuwa anataka kuhitimishwa utawala wa Putin.
Akizungumza hapo jana, Rais wa Marekani amedai kuwa mtu pekee wa kubeba lawama ni Rais Vladimir Putin wa Russia na akaongezea kwa kusema, Putin ameikaba demokrasia kwa kuishambulia kijeshi Ukraine.

Chaneli ya CNN imetangaza kuwa, hiyo ni kauli kali zaidi ya ukosoaji kutolewa na Biden dhidi ya Putin na inaonyesha mabadiliko makubwa katika muelekeo wa Marekani kuhusiana na Russia.
Kabla ya kauli hiyo ya Joe Biden, maafisa wa Marekani walikuwa wametangaza kuwa hawana lengo la kutaka kubadilisha utawala nchini Russia.
Wakati Rais Joe Biden wa Marekani alipotoa kwa mara ya kwanza kauli hiyo, kwamba Rais Vladimir Putin hapasi kubaki madarakani, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alimjibu kauli yake kwa kusema, rais na raia wa Marekani hawawezi kuamua kuhusu mtu wa kupasa kuweko madarakani nchini Russia na kwamba, raia wa Russia ndio wanaoweza kuamua hilo kwa kushiriki katika upigaji kura wa kumchagua rais wa nchi yao.../