EU: Mazungumzo ya Vienna yamefikia hatua nyeti na hasasi
(last modified Tue, 29 Mar 2022 07:55:48 GMT )
Mar 29, 2022 07:55 UTC
  • EU: Mazungumzo ya Vienna yamefikia hatua nyeti na hasasi

Msemaji wa Kamisheni ya Ulaya amesema, mazungumzo ya Vienna ya kufufua mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA yamefikia hatua nyeti na hasasi.

Nabila Massrali ameeleza kuwa, mazungumzo ya Vienna yanayolenga kufufua Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA yanaendelea na yanakaribia hatua ya mwisho.

Kabla ya hapo, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, alidokeza kuhusu mazungumzo ya uondoaji vikwazo ilivyoekewa Iran na akasema: "serikali ya Donald Trump ilifanya makosa kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran."

Borrell aliongezea kwa kusema: "tumekaribia kwenye mwafaka wa nyuklia na Iran na tumeshakubaliana kwa asilimia 95 katika nukta zote."

Hayo yanajiri katika hali ambayo, siku ya Jumapili waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alidai kuwa, Ulaya iliendeleza makubaliano ya nyuklia ya Iran licha ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano hayo. Le Drian alitamka hayo pasi na kuashiria jinsi pande za Ulaya zilivyohalifu ahadi zilizokuwa zimetoa za kuchukua hatua za kufidia madhara ambayo Iran ilipata baada ya Washington kujitoa katika JCPOA.

Karibu wiki mbili nyuma, pande husika katika mazungumzo ya Vienna zilitangaza kuwa, mazungumzo yamesitishwa; na jumbe za pande zote zimerudi kwenye miji mikuu yao kwa mashauriano. Hata hivyo Mkuu wa Sera za Nje wa EU, Josep Borrell alisema, mazungumzo hayo yamesitishwa kutokana na kile alichokiita "sababu za nje".

Borrell alikataa kuzitaja sababu hizo, lakini Iran ilitangaza kuwa kuibua Marekani matakwa mengine mapya na baadhi ya hatua zilizochukuliwa ikiwemo ya kuizuia meli ya mafuta ya Iran vimetatiza mazungumzo hayo ya Vienna.../

Tags