Waislamu wapinga mahakamani marufuku ya vazi la hijabu shuleni India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81948-waislamu_wapinga_mahakamani_marufuku_ya_vazi_la_hijabu_shuleni_india
Wanaharakati wa mawakili wa Kiislamu nchini India wameenda katika Mahakama ya Kilele ya jimbo la Kusini mwa India la Karnataka, kuukatia rufaa uamuzi wa Mahakama ya Juu kuidhinisha marufuku ya vazi la hijabu katika shule na vyuo vikuu vya jimbo hilo.
(last modified 2025-10-23T05:45:52+00:00 )
Mar 30, 2022 07:05 UTC
  • Waislamu wapinga mahakamani marufuku ya vazi la hijabu shuleni India

Wanaharakati wa mawakili wa Kiislamu nchini India wameenda katika Mahakama ya Kilele ya jimbo la Kusini mwa India la Karnataka, kuukatia rufaa uamuzi wa Mahakama ya Juu kuidhinisha marufuku ya vazi la hijabu katika shule na vyuo vikuu vya jimbo hilo.

Bodi ya Wanasheria wa Kiislamu nchini India imesema uamuzi wa mahakama ya nchi hiyo kuidhinisha rasmi marufuku ya Hijabu unakiuka haki ya kikatiba ya Wasichana Waislamu kuvaa vazi linaloaendana na mafundisho ya dini yao shuleni.

Taasisi hiyo ya mawakili wa Kiislamu nchini India imesisitiza kuwa, marufuku dhidi ya hijabu shuleni inahujumu moja kwa moja haki na uhuru wa kuabudu kwa wasichana na wanawake wa India.

Katikati ya mwezi huu wa Machi, Mahakama ya Juu ya jimbo la Kusini mwa India la Karnataka iliidhinisha rasmi marufuku ya vazi la hijabu katika shule na vyuo vikuu vya jimbo hilo, licha ya malalamiko na maandamano ya kupinga hatua hiyo.

Wanawake Waislamu India wakiandamana kulaani marufuku ya hijabu

Tangu mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2021, uvaaji wa vazi la staha la Kiislamu la hijabu umezusha mvutano katika jimbo la Karanatka. Skuli kadhaa za jimbo hilo zilijichukulia uamuzi wa kupiga marufuku uvaaji wa vazi hilo kwa wanafunzi wa kike.

Katika miaka ya karibuni, serikali ya waziri mkuu wa India Narendra Modi imewawekea mibinyo na vizuizi vikubwa Waislamu wa nchi hiyo.