Waislamu wa India wapeleka mahakamani mabuldoza hatari ya kisiasa
Jumuiya mashuhuri ya Kiislamu imewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya India, ikiitaka kuingilia kati baada ya matingatinga na serikali kuharibu mali na milki za Waislamu wanaotuhumiwa kuhusika na ghasia katika majimbo yanayoongozwa na chama cha Waziri Mkuu, Narendra Modi cha Bharatiya Janata Party (BJP).
Rais wa kundi la Jamiat Ulama-e-Hind, Arshad Madani, ameesema leo Jumatatu kwamba kundi hilo limewasilisha ombi katika Mahakama Kuu dhidi ya siasa hatari za tingatinga ambazo zimeanza kuharibu mali na milki za watu wa jamii za waliowachache, hasa Waislamu, kwa kisingizio cha kuzuia uhalifu katika majimbo yanayotawaliwa na BJP.
Ombi hilo linaitaka Mahakama Kuu ya India kutoa maagizo kwa serikali ya shirikisho na majimbo kwamba "hatua za kudumu za haraka zisichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa yeyote katika kesi yoyote ya jinai" na kwamba majengo ya makazi ya raia yasibomolewe kama hatua ya adhabu.
Wiki iliyopita, mamlaka katika majimbo yasiyopungua mawili ya India zilibomoa makumi ya nyumba na maduka, karibu yote ya Waislamu waliotuhumiwa kuhusika na vurugu wakati wa tamasha la Kihindu.
Katika jimbo la kati la Madhya Pradesh, ghasia zilizuka wakati wa tamasha la Ram Navmi mapema mwezi huu.
Kwa kawaida Wahindu hufanya maandamano makubwa siku ya kusherehekea kuzaliwa kwa mungu wao, Ram.
Hata hivyo, sherehe za mwaka huu za Wahindu zilishuhudia wanaume wa Kihindu waliovalia skafu za rangi ya zafarani wakiwa wamebeba mapanga, fimbo na bastola walipokuwa wakipita katika vitongoji hasa vya Waislamu, huku wakitishia kufanya mauaji ya kimbari katika jamii hiyo ya Waislamu na wakipiga muziki kwa sauti kubwa nje ya misikiti. Wahindu hao pia walishambulia nyumba na maduka ya Waislamu.

Katika wilaya ya Khargone huko Madhya Pradesh, ghasia zilizuka baada ya karibu nyumba 10 na msikiti mmoja kuchomwa moto wakati wa maandamano ya Ram Navmi, na kuwalazimu polisi kuweka amri ya kutotoka nje. Ghasia pia ziliripotiwa katika majimbo mengine ya India wakati wa tamasha hilo.
Katika miaka ya karibuni, serikali ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi imezidisha mibinyo na ukandamiza mkubwa dhidi Waislamu wa nchi hiyo.