Wataliano waandamana kulaani mashambulizi dhidi ya Wapalestina al-Aqsa
Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Italia, Rome ya kulaani mashambulio ya wanajeshi makatili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa al-Aqsa ulioko katika mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Katika maandamano hayo ya jana Jumatatu, waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za Palestina walilisikika wakipiga nara za kulaani chokochoko hizo mpya za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wananchi wa Italia katika maandamano hayo ya jana yalikuwa na jumbe za kulaani hujuma dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na matukufu ya Kiislamu.
Katika mkutano wa Disemba iliyopita kati ya Riyad al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina na mwenzake wa Italia, Luigi Di Maio, serikali ya Rome ilisisitiza kuwa itaendelea kuunga mkono Mamlaka ya Ndani ya Palestina,
Katika hatua nyingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya kikao cha dharura leo Jumanne, kujadili mzozo na makabiliano katika mji wa Quds. Mkutano huo utakaofanyika faraghani umeitishwa na China, Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu, Norway na Ireland.
Mapema Ijumaa iliyopita, wanajeshi wa Israel, wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni, walishambulia tena Msikiti wa al-Aqsa na kuwajeruhi Wapalestina wasiopungua 200 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala.
Wapalestina wengine zaidi ya 400 walitiwa nguvuni katika wimbi hilo jipya la mashambulio ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.