Siku ya Kimataifa ya Quds; ubunifu wa kuhuisha kadhia ya Palestina
(last modified Sat, 30 Apr 2022 03:09:57 GMT )
Apr 30, 2022 03:09 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Quds; ubunifu wa kuhuisha kadhia ya Palestina

Jana tarehe 29 Aprili ilisadifiana na mwezi 27 Ramadhani ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu, siku ambayo ni maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Ubunifu huo wa Imam Khomeini aliufanya miezi sita tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979.

Lengo kuu la ubunifu huu ni kuhuisha kadhia ya Palestina katika kiwango cha ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo swali la kimsingi linaloulizwa ni kwamba, Siku ya Kimataifa ya Quds inasaidia vipi mapambano ya ukombozi wa Palestina na kuifanya kadhia hiyo ibakie hai?

Kwanza kabisa, wakati Imam Khomeini anaitangaza na kuichagua Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kulikuwa kumejitokeza aina fulani ya kukata tamaa baina ya mataifa ya Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina. Sababu ya hilo ni kwamba, nchi za Kiarabu zilikuwa zimeshindwa mtawalia katika vita vyao na utawala ghasibu wa Israel, na madola makubwa yenye nguvu ya Magharibi yalikuwa yakiuunga mkono utawala huo kwa hali na mali.

Ubunifu wa kuweko Siku ya Kimataifa ya Quds ulilifanya suala la himaya na uungaji mkono kwa kadhia ya Palestina liendelee kuwepo miongoni mwa wananchi na muqawama wa wananchi. Wananchi wa mataifa mbalimbali hata yasiyokuwa ya Kiislamu wakatangaza mshikamano wao na taifa madhulumu la Palestina. Wapalestina nao kwa kadiri walivyoweza na kwa nguvu zao zote, wakaanzisha uhamasishaji mkubwa wa kuitetea na kuiokoa Baytul-Muqaddas kutoka katika makucha ya Wazayuni maghasibu.

Mintarafu hiyo, kwa mara nyingine tena kadhia ya Palestina ikawa imehuishwa na kubakia hai hadi leo. Baada ya kupita miongo kadhaa na licha ya baadhi ya mataifa ya Karabu kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na adui Mzayuni na hata kuweko propaganda za kila upande za vyombo vya habari vya Wamagharibi dhidi ya Palestina na kuipendelea Israel, lakini yote haya hayajalifanya suala la Palestina lisahaulike. Hii leo wananchi wa Palestina wameshadidisha muqawama na mapambano yao dhidi ya utawala vamizi wa Israel.

Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina anasema: Muqawama na mapambano ya taifa la Palestina na utayari uliopo katika muqawama wa Lebanon sambamba na maneno ya kimapinduzi ya Iran ni mambo ambayo yametupa hakikisho kwamba, tutapata ushindi. Iran daima imekuwa ikiunga mkono haki, Palestina na Quds.

Pili, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kulianzishwa asasi na jumuiya za kiraia za Palestina na zisizo za Palestina kwa ajili ya kuiunga mkono Palestina na mapambano dhidi ya utawala vamizi wa Israel. Harakati ya Jihadul Islami, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni miongoni mwa asasi na harakati hizo. Ukweli wa mambo ni kuwa, harakati hizo ni matunda na natija ya ubunifu wa Siku ya Quds. Harakati hizo zilianzishwa kwa himaya ya wananchi na zikaufanya msingi na nguvu zao kuwa ni wananchi.

Fikra hii ikawa sababu ya muqawama kuchukua wigo mpana baina ya wananchi. Kuenea fikra ya muqawama katika nchi nyingine kumeifanya azma ya Wapalestina ya kukabiliana na jinai za Israel iwe maradufu na hata kuwafanya wawe na matumaini ya kupata ushindi mkabala wa Wazyuni na hivyo kuzikomboa ardhi zao na vilevile kuweza kuulinda msikiti wa al-Aqswa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Tatu, ubunifu wa Siku ya Quds katika dhati yake una hali ya kujiimarisha na kupata nguvu. Kwani kulifanya suala la Palestina kuwa hai kimsingi bila ya kujiimarisha na kupata nguvu ni jambo ambalo haliwezekani.  Mbali na uungaji mkono na harakati za wananchi za kufichua dhulma dhidi ya Palestina na jinai za utawala haramu wa Israel, kuna haja pia ya kuweko misingi ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa maneno mengine ni kuwa, fikra iliyojikita kwa Wapalestina ni hii kwamba, njia ya kupambana na kutetea ardhi zao ni kujiimarisha na kuwa na nguvu zaidi na siyo kutegemea mataifa mengine kuendesha mapambano kwa ajili ya Palestina. Brigedi za matawi ya kijeshi ya makundi mbalimbali ya Palestina zimeanzishwa na kuimarisha uwezo wao wa kijeshi.

Ni kwa msingi huo, ndio maana tunaona kuwa, Wapalestina wametoka katika hatua ya kupambana kwa kutumia mawe na kufikia hatua ya kupambana kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani. Huku kujiimarisha na kuwa na nguvu kumedhihirisha udhaifu na kuweza kudhurika utawala wa Kizayuni. Kuchezea vipigo Israel kumeyafanya matumaiani ya Wapalestina ya kupata ushindi kuongezeka siku baaada ya siku. Bilas haka hii ni natija ya kuendelea kuweko ubunifu wa Imam Khomeini wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.