Jan 22, 2026 03:10 UTC
  • Leo ni Alkhamisi, tarehe 22 Januari, 2026

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Shaaban 1447 Hijria sawa na Januari 22 mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1051 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria, Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afganistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. 

Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Monajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". 

Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."   

Siku kama ya leo miaka 465 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561 alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon.

Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya.

Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626. 

Miaka 251 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa.

Akiwa kijana mdogo alipendelea sana taaluma ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836.   

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malkia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64.

Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ulikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII.   

Miaka 47 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, ikiwa ni katika mwendelezo wa wananchi Waislamu wa Iran kupinga utawala wa Shah na kukabiliana na wanajeshi wa utawala huo, idadi kubwa ya raia  waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Wananchi wa  Iran ya Kiislamu wambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kurejea nchini Imam Khomeini (M.A) walitayarisha mazingira hitajika kwa ajili ya mapokezi makubwa zaidi ya kihisitoria kwa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mnasaba huo, wafanyakazi mbalimbali wakiwemo maulamaa na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wakazi wa mji wa Tehran walikusanyika pamoja ili kuandaa hafla kubwa ya kumpokea Imam. 

Watu wengi kutoka katika miji na vijiji vya Iran ya Kiislamu walimiminika kwa wingi mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika sherehe za kumkaribisha Imam Khomeini (M.A).

Katika upande mwingine, baada ya maandamano makubwa ya wananchi, wanajeshi elfu nne wa jeshi la anga pia waligoma kula wakitaka kuondoka Iran washauri wa kijeshi wa Marekani katika kuwaunga mkono wananchi wanapambano wa Iran.   

Na tarehe 22 mwezi Januari mwaka 1979 ; miaka 47 iliyopita mwanamapambano wa Kipalestina Abu Hassan Salameh aliuawa kigaidi na maajenti wa utawala wa Kizayuni.

Abu Hassan Salameh ndiye aliyepanga na kuratibu oparesheni ya kuwateka nyara  Waisraili 12 katika mashindano ya Olimpiki huko Munich Ujerumani mwaka 1972. Salameh alikuwa Kamanda  wa Jeshi la Vita Vitakatifu vya Palestina katika Vita vya Palestina vya  mwaka 1948. Oparesheni hiyo ilitekelezwa Septemba 5 mwaka 1972 na kupelekea kuuawa mateka 12 wa Israel, Wapalestina 5, polisi mmoja wa Ujerumani na kutiwa nguvuni Wapalestina 3.

Abu Hassan ndiye aliyepanga  oparesheni hiyo japokuwa mwenyewe hakushiriki moja kwa moja kwenye oparesheni hiyo. Abu Hassan Salameh aliuliwa kigaidi Januari 22 mwaka 1979 miaka saba baada ya oparesheni ya Munich. Aliuawa katika moja ya mitaa ya Beirut akiwa na wenzake wanne wakati walipotoka nje ya nyumba baada ya kuripukiwa na bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari mkabala wa nyumba yake.