Wasiwasi wa kuongezeka utumiaji mabavu unaotokana na ubebaji silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i84236-wasiwasi_wa_kuongezeka_utumiaji_mabavu_unaotokana_na_ubebaji_silaha
Sambamba na kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu vinavyotokana na umiliki kiholela na ubebaji silaha nchini Marekani, kumeibuka wasiwasi mkubwa katika mataifa jirani na Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 01, 2022 01:19 UTC
  • Wasiwasi wa kuongezeka utumiaji mabavu unaotokana na ubebaji silaha

Sambamba na kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu vinavyotokana na umiliki kiholela na ubebaji silaha nchini Marekani, kumeibuka wasiwasi mkubwa katika mataifa jirani na Marekani.

Wasiwasi huo umekuwa mkubwa kiasi kwamba, katika hatua yake ya hivi karibuni serikali ya Canada imewasilisha muswada ambao kwa mujibu wake uuzaji na ununuaji silaha utasimamishwa na uuzaji wa vidude na vifaa vya kuchezea watoto ambavyo vinafanana na silaha nao utapigwa marufuku.

Lengo la muswada huu ni kusimamisha uuzaji na ununuzi wa bastola ikiwa ni sehemu ya kudhibiti umiliki wa silaha na vilevile kupiga marufuku uuzaji wa baadhi ya vidude vya kuchezea watoto ambavyo vinashabihiana na silaha. Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada ametangaza kuwa, hatua hizi mpya ni za lazima hasa kwa kuzingatia kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu kwa kutumia silaha.

Muswada huo mpya unawasilishwa na serikali ya Canada katika hali ambayo, siku chache zilizopita skuli kadhaa nchini humo zilifungwa kutokana na tishio la ufyatuaji risasi

Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, wiki chache zilizopita, serikali ya Canada ilichukua hatua ya kukaza sheria za kununua silaha kihalali. Kwa mujibu wa sheria mpya, mashirika ya uuzaji silaha pamoja na mambo mengine yanapaswa kusajili idadi ya silaha moto zilizoko katika maghala na stoo zao.

Kushtadi na kuchukua wigo mpana vitendo vya utumiaji mabavu katika mataifa ya Magharibi hususan Marekani ni jambo ambalo kivitendo limeyafanya maisha ya raia wengi hususan watoto na wanafunzi wa shule kuwa hatarini. Hili ni jambo ambalo limezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa watu hasa katika mataifa yanayopakana na Marekani hususan Canada.

Uchunguzi uliofanywa na Idara ya Usalama wa Umma unaonyesha kuwa, asilimia 47 ya wananchi wa Canada wanaamini kuwa, jamii yao inakabiliwa na hatari ya vitendo vya mabavu kwa kutumia silaha. Aidha utafiti uliofanywa na Asasi ya Leger and Association for Canadian Studies mwaka uliopita (2021) unaonyesha kuwa, takribani 66% ya wananchi wa Canada wanapinga kupasishwa sheria ya kumiliki silaha huku 19% tu wakiwa ni wafuasi wa sheria inayoruhusu kumiliki na kutembea na silaha.

Waziri Mkuu wa Canada amekiri kuwa, inatosha tu kutazama mpaka wa kusini ili tudiriki kwamba, kama hatutachukua hatua madhubuti na za haraka, hali ya mambo itakuwa mbaya zaidi katika sikku za usoni ambapo kukabiliana nayo wakati huo litakuwa jambo gumu.

Mauaji ya ufyatuaji risasi katikak jimbo la Texas nchini Marekani

 

Maamuzi hayo ya Canada yanatangazwa katika hali ambayo, wiki iliyopita Marekani ilishuhuudia moja ya mauaji mengine ya kutisha ya ufyatuaji risasi. Watoto wadogo wasiopungua 19 waliuawa kwa umati baada ya gaidi mmoja aliyetajwa kwa jina la Salvador Ramos kuvamia shule yao huko Uvalde Texas Marekani. Tukio hilo ni mlolongo wa matukio ya mauaji ya ufyatuaji risasi katika miezi ya hivi karibuni katika shule nchini Marekani. Mauaji hayo yalipelekea maelfu ya Wamarekani kuandama na kulalamikia sheria mbovu za nchi hiyo katika suala zima kumiliki silaha.

Seneta Chris Murphy wa chama cha Republican amekiri kwamba, kununua silaha nchini Marekani ni rahisi mno kuliko hata kununua mnyama wa kufuga. Aliongeza kusema kuwa, usalama wa kiakili na kisaikolojia siyo sababu pekee ya matukio ya simanzi ya ufyatuaji risasi na mauaji katika shule za nchi hiyo, bali upatikanaji kirahisi na umiliki kiholela wa silaha nchini humo ni jambo ambalo limekuwa na taathira kubwa katika matukio ya mauaji na ufyatuaji risasi katika skuli za Marekani.

Seneta Chris Murphy wa chama cha Republican amekiri kwamba, kununua silaha nchini Marekani ni rahisi mno kuliko hata kununua mnyama wa kufuga

 

Filihali baada ya vitendo vya mabavu kwa utumiaji silaha kuchukua wigo mpana nchini Marekani, kumezuka wasiwasi mkubwa katika mataifa yanayopakana na Marekani huku serikali husika zikiwa mbioni kuhakikisha kwamba, zinapasisha sheria za kukabiliana na mwenendo huu.

Hii ni katika hali ambayo, inaonekana kuwa, kwa kuzingatia utamaduni unaotawala katika mataifa hayo na kuongezeka malalamiko ya kijamii na kiutamaduni, kuchukuliwa hatua kama hizo kutakuwa na taathira chanya.