Aug 26, 2025 02:41 UTC
  • Jumanne, tarehe 26 Agosti, 2025

Leo ni Jumanne tarehe Pili Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na tarehe 26 Agosti 2025.

Siku kama ya leo miaka 817 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi.

Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu.

Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7,500 wa Mtume Muhammad (saw).

Katika siku kama ya leo miaka 679 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia.

Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa.

Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga.

Miaka 282 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Ufaransa Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa.

Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali.

Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye. 

Antoine Laurent Lavoisiere

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia.

Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano.

Katika siku kama hii ya leo miaka 46 iliyopita tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mehdi Araghi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO). Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alifanya mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah. Mehdi Araghi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi.

Mehdi Araghi (kulia) akiwa pamoja na Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali.

Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.